Mbowe ashtukia jambo CHADEMA

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 09:20 AM Dec 23 2024
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amerejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya uenyekiti wa chama hicho huku akitoa angalizo kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho kutotumia uchaguzi huo kuharibu taswira ya chama.

Ameagiza mamlaka za chama zinazohusika kusimamia uchaguzi huo, zihakikishe unakuwa huru na wazi ili usiwe na doa. Atakayeshinda awe na uhalali mbele ya wanachama wa chama hicho.

"Ninaagiza mamlaka za chama zinazohusika na kusimamia mkakati wote ama mchakato wote wa uchaguzi pamoja na uchaguzi wenyewe, zihakikishe uchaguzi wetu unakuwa safi usiokuwa na doa, uwe wazi, kila mtu aone, dunia ione kwamba CHADEMA tunaweza kuchaguana bila kufanya wizi wa kura kwa sababu wizi si asili yetu," alisema Mbowe baada ya kurudisha fomu katika ofisi za chama hicho Dar es Salaam jana.

Mbowe aliongeza: "Yeyote atakayepatikana akawe na uhalali mbele macho ya wana-CHADEMA, mbele ya macho ya dunia na zaidi mbele ya macho ya Mungu. Ninawaombea sana wale ambao watashindana katika kampeni, ninarudia mara kwa mara, kafanyeni kampeni za kuijenga taasisi yetu na msijenge kampeni za kuumizana kwa mambo ambayo si ya kweli.

"Tukawe watu wa kweli wa kukilinda chama chetu, viongozi, kulinda wagombea na wanachama wetu. Sisi ni familia, u-familia wetu hauwezi ukafa kwa sababu ya uchaguzi."

Mbowe alisema anatamani ijengwe CHADEMA yenye ustahimilivu, yenye viongozi wanaoweza kukutana na changamoto lakini wakawa wastahimilivu. 

"Tunatamani tukaijege CHADEMA yenye viongozi wabunifu, tukafanye mabadiliko yote tunayofikiri yakifanywa yatakifanya chama chetu kuwa bora zaidi katika malengo yetu ya kupigania haki ya watu wake, uhuru wa watu wake, demokrasia ya watu wake na hatimaye maendeleo ya watanzania wote katika ujumla wake," alisema.

Mbowe alitoa tahadhari kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao tayari wameshaanza kutoka nje ya mstari kwenye kampeni zao kuelekea uchaguzi huo na kwamba wanawaombea ili wafanye kampeni za kistaarabu na si za kupasua chama au kuumizana. 

"Tunatambua kuna wengine ambao wanatoka nje ya mstari katika kutengeneza kampeni chafu za matusi, hiyo si tamaduni wala si tabia ya CHADEMA, tunawaomba wale wote waliopendekeza kampeni za kutugawa, basi wakapate busara ya kuachana na kampeni za kutugawa. 

Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Januari mwakani. Nafasi zinazogombaniwa ni pamoja na ya Mwenyekiti wa Chama Taifa, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar.

Nyingine ni Katibu Mkuu Baraza la Wazee (BAZECHA) Bara, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Mwekahazina.

Pia zipo za wajumbe watano wa Baraza Kuu ambao wanne kutoka Tanzania Bara na mmoja kutoka Tanzania Zanzibar pamoja na wajumbe 20 wa mkutano mkuu ambao 15 ni wa kutoka Tanzania Bara na watano ni kutoka Tanzania Zanzibar.