Dk. Mwinyi azindua miradi mitano ya kuongeza ufanisi viwanja vya ndege

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:57 AM Dec 23 2024
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mtandao
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, uimarishaji miundombinu katika viwanja vya ndege, unalenga kuvifanya kuwa bora na kutoa huduma kulingana na vigezo vya kimataifa.

Alitoa kauli mwishoni mwa wiki alipozindua miradi mitano ya miundombinu mbalimbali katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wilaya ya Magharibi B, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema lengo ni kuwa na viwanja vya ndege vyenye sifa ya utoaji huduma bora kwa abiria zitazokidhi mahitaji ya ongezeko la wageni wanaoingia nchini kila siku.

Alisema miradi mitano aliyozindua itafanya uwanja huo kuwa wa kujivunia na hadhi ya kimataifa katika Afrika na duniani kwa  utoaji huduma bora zitakazoridhiwa na  wageni.

Miradi aliyozindua Dk. Mwinyi ni pamoja uwekaji mawe ya msingi kwa majengo ya abiria 'Termninal One' na 'Two', ambayo alisema itajumuisha ujenzi wa jengo la viongozi na wageni mashuhuri (VIP) utakaotumiwa pia na wafanyabiashara wakubwa kupokea ndege binafsi za wageni mashuhuri.

Akizungumzia ujenzi wa kituo cha kisasa cha biashara, Rais Dk. Mwinyi alisema utahusisha majengo ya benki, migahawa mikubwa ya kimataifa na ofisi zitakazotoa huduma saa 24 kwa wageni na watumiaji wa uwanja huo pamoja na uzinduzi wa taa mpya za kuongozea ndege na mradi wa kituo cha mafuta ya ndege.

Rais Dk. Mwinyi alisema kituo hicho cha mafuta kitaleta ushindani katika utoaji huduma za mafuta kwa ndege zinazotua uwanjani huko na kutoa unafuu wa bei na kupunguza safari za ndege kwenda kuweka mafuta nje ya Zanzibar.

Akizungumzia Uwanja wa Ndege wa Pemba, Rais Mwinyi alisema serikali imekusudia kuujenga kuwa wa kimataifa kwa kuutanua na kuongeza njia za kuruka na kutua ndege ili kuifungua Pemba kibiashara.

Alisema Pemba ijayo itapokea wageni na watalii moja kwa moja badala ya kushuka Zanzibar na hatimaye kuunganisha ndege nyingine kwenda Pemba. Alisema mradi huo unatekelezawa sambamba na ujenzi wa bandari za Mkoani, Wete na Shumba Mjini ili kuikuza Pemba kwa utalii, biashara na uwekezaji.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuridhishwa kwake na kazi kubwa inayofanywa na Mamkala ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) hususan mabadiliko ya utendaji yanayozingatia uwajibikaji na nidhamu, pia kusifu juhudi kubwa wanazofanya wafanyakazi wa mamlaka hiyo kuufanya uwanja huo kupokea wageni wengi zaidi.

Akizungumzia ukuaji wa utalii nchini, Rais alisema takriban watalii milioni mbili wanaingia nchini kila mwaka, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua juhudi maalumu za kuimarisha viwanja vya ndege kwa miundombinu bora.

Rais Dk. Mwinyi aliahidi ujenzi wa hoteli kubwa zenye hadhi ya juu ili kuwavutia wageni wengi zaidi, hatua itakayoimarisha utalii na kuongeza mapato yanayotokana na sekta huyo muhimu kiuchumi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa busara na miongozo anayotoa kwa wizara hiyo ambayo imechangia maendeleo makubwa ya viwanja vya ndege nchini na kumpongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwaletea maendeleo Wazanzibari.

Pamoja na kusifia kazi kubwa inayofanywa na ZAA hadi kupata tuzo za kimataifa kufuatia mabadiliko ya utendaji katika mamlaka hiyo ya utoaji wa huduma bora.

Mkurugenzi Mkuu wa ZAA, Seif Abdalla Juma alisema ujenzi wa majengo ya abiria 'Terminal One' na 'Two' na kituo cha kisasa cha biashara yanagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema ujenzi umefikia hatua nzuri na kuongeza kuwa umetokana na kuchakaa kwa majengo ya zamani ambayo hayaendani na mahitaji ya sasa ya mabadikilo ya viwanja vya ndege duniani.

Alisema mbali ya mabadiliko makubwa uwanjani huko, wanakusudia kuweka mfumo wa kisasa wa kuhifadhi makontena ya mizigo kwa lengo la kuendana na mahitaji na ubora wa viwanja vya sasa vya ndege duniani.