Video ya mwanamke yawaponza wapigaji makachu wa Forodhani

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:17 AM Dec 23 2024
Video ya mwanamke yawaponza wapigaji makachu wa Forodhani
Picha:Mtandao
Video ya mwanamke yawaponza wapigaji makachu wa Forodhani

MAMLAKA ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe Zanzibar imetangaza kusimamisha shughuli za upigaji mbizi baharini, maarufu makachu, katika eneo la Forodhani.

Mamlaka hiyo imetoa taarifa hiyo kufuatia matukio ya ukiukwaji wa sheria, kanuni na miongozo yaliyojitokeza kwa vijana wa makachu katika eneo la bustani ya Forodhani na kuleta athari mbaya kwa jamii na miundombinu ya serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo jana kupitia kitengo cha habari na uhusiano, matukio hayo yanajumuisha upigaji makachu kwa kutumia mavazi yanayokwenda kinyume cha utamaduni, uharibifu mkubwa wa mifereji na miundombinu mengine.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kufuatia matukio hayo, mamlaka imesimamisha shughuli hizo za makachu hadi hapo itakapokamilisha kuandaa utaratibu wa kuimarisha usimamizi wa shughuli hizo.

Mamlaka hiyo inasema katika taarifa yake hiyo kuwa serikali inatambua mchango wa makachu kutangaza utalii na mamlaka hiyo inaendelea na uchunguzi wa jambo la ukiukwaji maadili na wahusika watakapobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibu katika mitandao ya kijamii kulisambazwa video ikimwonesha mwanamke akiruka makachu katika eneo la Forodhani akiwa na nguo za ndani tu huku maumbile yake yakiwa yanaonekana, jambo ambalo liliibua taharuki kwa wananchi, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu.

"Mamlaka kwa kushirikiana na wadau na watumiaji wa Mji Mkongwe inaziomba taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi wote kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo kama hivyo ili wachukuliwe hatua.

"Kwa pamoja tunaweza kulinda na kuendeleza mji huo ambao ni urithi wetu wa kihistoria na kiutamaduni," mamlaka hiyo inaeleza katika taarifa yake hiyo.

Kabla ya kutolewa taarifa hiyo, Balozi Mdogo wa Brazil, Abdulbasit Abdulsamad, alilaani tukio hilo ambalo alisisitiza halileti taswira nzuri kwa Zanzibar na linakwenda kinyume cha maadili ya wazanzibari.

Shughuli za upigaji makachu katika eneo hilo la Forodhani zimeijengea umaarufu mkubwa Zanzibar katika mataifa mbalimbali duniani na kuitangaza kiutalii. Wageni wengi humiminika katika eneo hilo kujionea na wengine kushiriki shughuli hiyo ambayo imeongeza ajira kwa vijana.