Yanga, Simba bado mna nafasi kufuzu robo fainali ya CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:04 AM Dec 14 2024
Yanga, Simba
Picha:Mtandao
Yanga, Simba

WAKATI Yanga leo itajitupa kwenye Uwanja wa Lubumbashi, nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kucheza dhidi ya TP Mazembe kwenye mechi ya raundi ya tatu, Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, kesho Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Mechi hii ni ya raundi ya tatu, Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi. 

Kipigo cha mabao 2-0 ilichokipata Yanga dhidi ya MC Alger ya Algeria wiki iliyopita na mabao 2-1, ilichokipata Simba dhidi ya CS Conastantine kimewafanya baadhi ya mashabiki wa timu hizo waanze kukata tamaa ya kupita katika hatua ya makundi.

Baada ya mechi hizo, hata ukisoma kwenye mitandao ya kijamii,  baadhi wanaonekana kukata tamaa kuwa inawezekana msimu huu timu zao zisiweze kupita hatua ya makundi na kwenda robo fainali.

Ni kwa sababu Yanga mpaka kufikia raundi ya pili haina pointi hata moja, lakini Simba pamoja na kwamba ina pointi tatu, lakini kiwango inachokionyesha kimeonekana kutowaridhisha baadhi ya mashabiki wake.

Niwaambie tu mashabiki wa soka nchini kuwa ni mapema mno kuzikatia tamaa timu hizo kwa sasa.

Iwapo Yanga itashinda mchezo wa leo, itakuwa imerudi kwenye reli na itakuwa imebakisha mechi mbili nyumbani na moja ugenini, hivyo chochote kinaweza kutokea.

Niwatoe wasiwasi wanachama na mashabiki wa timu hizi waendelee kuzisapoti timu zao waendelee kujitokeza viwanjani kama mechi inachezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuwatia nguvu wachezaji.

Mara nyingi mashabiki wa soka nchini hawana tabia ya kwenda kujazana uwanjani kama timu zao zinafanya vibaya. Hii inaweza kufifisha juhudi za viongozi na wachezaji kutinga hatua ya robo fainali.

Ikumbukwe kuwa Simba ilipitia kipindi kigumu kama hicho, mfano tu msimu uliopita, ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, suluhu ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, baadaye ikafungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.

Hapa utaona kuwa kwenye michezo mitatu ilikuwa haijashinda hata mchezo mmoja, lakini ikapambana na kushinda mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca, kabla ya kulazimishwa suluhu kwa mara nyingine dhidi ya Asec Mimosas ugenini.

Hii inaonyesha kuwa Simba ilipita kwenye njia ngumu mno, kiasi kwamba mechi mbili za mwisho ililazimika kushinda zote, ikaifunga Jwaneng Galaxy mabao 6-0, na kutinga hatua hiyo.

Misimu mwili iliyopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo, ilionekana kama imeshatolewa kwenye kinyang'anyiro kwa kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi, lakini ilishinda michezo miwili mfululizo dhidi ya Vipers ya Uganda na kurejesha matumaini, kabla ya mchezo wa mwisho kuikandamiza Horoya mabao 7-0, ikatinga kwa kishindo robo fainali.

Mifano hii ni kuonyesha kuwa timu hizi zikikaa chini na kupiga hesabu zake vizuri, kuandaa mikakati ya ndani ya uwanja ya kiufundi ikichanganya na rasilimali watu ambao ni mashabiki wake kwa kuwahamasisha kujazana uwanjani kwenda kuzipa sapoti kama ilivyokuwa ikifanya Simba huko nyuma, ikipita mara kwa mara katika mazingira magumu, basi hakuna kitakachoshindikana.