MNAMO tarehe 11 mwezi huu, wanafunzi 529,321 wa Kidato cha Nne walianza kufanya Mtihani wa Taifa wa kidato hicho (CSEE). Kwa mujibu wa ratiba inamalizika kesho.
Cha ajabu ni kwamba wanafunzi 161,020 sawa na asilimia 23.3, hawakuwa miongoni mwa watahiniwa hao.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed, aliyoitoa wakati akitangaza kuanza kwa mtihani huo ni kuwa hali hiyo imebinika baada ya kuangalia idadi ya wanafunzi hao walipofanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha pili mwaka 2022 walikuwa ambapo 690,341, lakini walioandikishwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne 2024 ni 529,321.
Hii ni dalili mbaya kwenye sekta ya elimu, hivyo kuna haja ya wadau wa sekta hiyo pamoja na serikali kushirikiana kupata taarifa sahihi zizobainisha sababu za wananafunzi hao kushindwa kufanya mtihani huo, ili kuhakikisha jambo hilo halijitokezi tena.
Kiwango cha asilimia 23 ya wanafunzi hao kushindwa kufanya mtihani huo kinazua maswali kwa hakika, licha ya kwamba hata miaka iliyopita kuna idadi ya wanafunzi kadhaa walikwama kufanya mtihani hiyo kitaifa, kwa sababu mbalimbali zikiwamo zilizo nje ya uwezo wao wanafunzi husika au wazazi na walezi kama vile kuugua .
Katika andiko la Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 Toleo la Mwaka 2023, inaeleza tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 imeonyesha kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau, ilitekeleza afua mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa fursa za elimu na mafunzo kwa usawa.
Pia, inabainisha afua hizo ni pamoja na utoaji wa elimu bila ada kwa shule za awali, msingi na sekondari kupitia Waraka wa Elimu Namba Tatu ya mwaka 2016; Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi 2021/22-2025/26; Mwongozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatiza Masomo Katika Elimu ya Msingi na Sekondari kwa sababu Mbalimbali wa mwaka 2022.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, uandikishaji sekondari ya chini (kidato cha I-IV) ulitajwa kuongezeka kutoka 1,675,593 (wavulana 824767; wasichana 850,826) mwaka 2016 hadi 2,645,115 (wavulana 1,248,118; wasichana 1,396,997) mwaka 2022 na kidato cha 5-6 kutoka 131,362 (wavulana 81,129; wasichana 50,233) mwaka 2016 hadi 178,473 (wavulana 99,101; wasichana 79,372) mwaka 2022.
Imebainishwa katika sera hiyo kuwa, ili kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali, serikali imeweza kuwarejesha wanafunzi 8,652 masomoni, wanafunzi 6,685 (wasichana) walirejea kupitia utaratibu wa elimu nje ya mfumo rasmi na wanafunzi 1,967 (wavulana 861; wasichana 1,046) walirejea katika mfumo rasmi wa elimu kwa mwaka 2022/23.
Andiko hilo linabainisha kuwa elimu ya sekondari inakusudia kufikia malengo kadhaa ikiwamo kupanua, kuimarisha, na kuendeleza maarifa, stadi, na mtazamo chanya uliopatikana katika ngazi ya elimu ya msingi.
Pia, kuna kumwezesha mwanafunzi kuelewa na kulinda misingi ya utamaduni (mila na desturi), umoja wa kitaifa, tunu za Taifa; na kuthamini haki za binadamu na wajibu unaoendana na haki hizo.
Aidha, kuna suala la kujenga uelewa wa mwanafunzi kuhusu demokrasia, umuhimu na mipaka yake; kujenga utamaduni na umahiri kwa mwanafunzi katika kujisomea, kujiamini, kujiendeleza kwenye nyanja za sayansi na teknolojia, maarifa ya kinadharia, kiufundi, kiujasiriamali na kupenda kufanya kazi.
Aidha, kunatajwa; kumwezesha mwanafunzi kutumia stadi za lugha mbalimbali; kumwezesha mwanafunzi kutambua uwajibikaji wa pamoja wa kutunza afya, kuthamini usawa wa kijinsi na kusimamia utunzaji endelevu wa mazingira; kuimarisha misingi ya uadilifu na kuheshimu utawala wa sheria.
Kujenga ujuzi na stadi mbalimbali zitakazomwezesha mhitimu kujiunga na elimu ya juu na mafunzo ya amali sanifu baada ya elimu ya sekondari, kujiajiri, kuajiriwa, na kuyamudu maisha kwa kutumia mazingira yake.
Kutokana na maelengo yaliyoanishwa hapo, ndipo ninapoona haja ya kutambua mkwamo wa wanafunzi hao, kwa kuwa ni wazi idadi yao watakosa malengo hayo yaliyoainishwa hapo kwa kushindwa kumaliza elimu ya sekondari.
Malengo hayo ni mambo umuhimu, kuanzia binafsi,kwa jamii na taifa kwa ujumla. Naamini sababu zikijulikana, pia wataalam husika watashirikishwa ili kupata ufumbuzi wa kueleweka, ambao utasaidia kuzuia kutokea tena kwa mkwamo huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED