Karume: Usafirishaji dawa kulevya unaathiri uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:01 AM Jan 04 2025
Rais mstaafu Dk. Aman Karume.
Picha:Mtandao
Rais mstaafu Dk. Aman Karume.

RAIS mstaafu Dk. Aman Karume, amesema usafirishaji wa dawa za kulevya huathiri ukuaji wa uchumi na kusababisha kuwapo utakatishaji wa fedha haramu, rushwa na mfumuko wa bei katika nchi.

Karume aliyasema hayo huko Kidimni Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja alipozungumza katika uzinduzi wa kituo cha tiba na urekebishaji tabia kwa waathirika wa dawa za kulevya.

Alisema suala hilo pia linachangia kuwapo uzalishaji mdogo wa kipato unaotokana na kupungua kwa nguvu kazi ya taifa na ukosefu wa ajira.

Aidha, kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya jamii haina budi kuchukua hatua za kuimarisha malezi bora kwa watoto na kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa tabia za vijana ili kuwalinda na makundi hatarishi na kushiriki kuwapatia elimu ya athari zitokanazo na dawa za kulevya.

Alisema vijana wanaweza kujikinga na janga hilo kwa kushiriki kwenye michezo mbalimbali, kujiepusha na imani potofu na kuacha kuiga tabia zisizokubalika katika jamii na kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aliitaka mamlaka ya udhibiti na kuzuia dawa za kulevya Zanzibar kuendelea kuwa wakali ili kuwasaka na kuwakamata wahusika wote wanaojihusisha na dawa za kulevya na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria.

Alisema utafiti mbalimbali zilizofanywa duniani zinaonesha vijana wanapotumia dawa za kulevya wakiwa na miaka 15 wanakufa wakiwa na umri uziozidi miaka 25 jambo ambalo linapoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo.

Aliitaka jamii kukitumia kituo hicho kwa kuwalea watoto kupata tiba na kurekebishwa tabia na pia kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa walioachana na utumiaji wa uraibu huo wa dawa za kulevya, kuacha muhali na kuendelea kuwafichua wote wanaojiusisha na biashara ya dawa hizo ili kumaliza tatizo hilo Zanzibar.

Akitoa maelezo ya kitaalamu Katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bimaryam Juma Abdalla, alisema kituo hicho ni cha aina yake Afrika Mashariki na kina lengo la kuhakikisha kwamba kinawasaidia vijana kuondokana na matumizi ya dawa za kulevya na kufunzwa, ujasiriamali ikiwamo ushonaji, ufundi magari, ufugaji, uwashi na mambo mengine ili kuwasaidia vijana walioachana na tatizo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harous Said Suleiman, alisema kukamilika kwa kituo hicho muhimu katika kutoa huduma za matibabu na msititizo katika mapambano na kudhibiti tatizo la dawa za kulevya kukamilika kwa kituo hicho ni sehemu muhimu katika juhudi za serikali za kuleta maendeleo ya kupambana na tatizo la athari zinazotokana na dawa za kulevya Zanzibar.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanal Burhan Zubeir Nassoro, alisema pamoja na mafanikio makubwa ya kupambana na suala hilo, lakini kuna changamoto kadhaa ikiwamo baadhi ya wazazi kuwasusa watoto wao licha ya kuacha uraibu huo na baadhi ya waraibu kutopenda kujiunga na kazi za ujasiriamali na stadi za kazi.

Hivi sasa Zanzibar inakisiwa kuwa na idadi ya vijana wapato 10,000 wanajihusisa na matumizi ya dawa za kulevya na kusababisha athari kubwa kwao binafsi, familia na jamii kwa jumla.