KAMATI za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinatarajia kujifungia Dodoma kwa siku 18 kwa shughuli maalum ikiwamo kuchambua miswada ya sheria.
Kamati hizo pia zitachambua sheria ndogo, kupokea taarifa za utendaji wa serikali na taasisi zake, kuchambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma jana ilieleza kuwa vikao hivyo vinatarajiwa kuanza Januari 6 hadi 24 mwaka huu vikifuatiwa na Mkutano wa 18 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 28,mwaka huu..
Taarifa hiyo ilitaja kamati zitakazoanza kufanya vikao hivyo kuwa ni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo siku ya Januari 6 kisha kamati nyingine zitafuata Januari 13.
Aidha ilieleza kuwa kamati mbili zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2023.
Ilisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma kuangazia kama ili uwekezaji wake umezingatia taratibu na miongozo ya biashara.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo itachambua Sheria Ndogo,
Ilisema pia za Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Maji na Mazingira na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) zitachambua miswada ya sheria.
Ilisema pia kamati 11 za kisekta zitapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji wa Serikali na Taasisi zake.
Aidha, Kamati ya Bajeti itapokea na kujadili taarifa kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2024).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED