Kamati ya Waamuzi tujuzeni sasa hatima suala la Kayoko

Nipashe
Published at 08:13 AM Dec 09 2024
TFF
TFF
TFF

BAADA ya kuchezesha mechi ya dabi ya Simba na Yanga, Oktoba 19, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, iliyokuwa na maamuzi mengi yenye utata, mwamuzi Ramadhani Kayoko hajaonekana tena uwanjani.

Hajaonekana kuchezesha mechi yoyote kitu ambacho si cha kawaida, kwani inakaribia miezi miwili sasa, kwa mwamuzi kama yeye angekuwa angalau tumemwona akichezesha walau hata mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo wa Oktoba 19, ambao Yanga ilishinda bao 1-0, kulikuwa na maamuzi mengi ya kufikirisha, ambapo kwa mujibu wa baadhi ya viongozi wa Simba, wachambuzi, pamoja na marudio ya video, kulikuwa na matukio ya mchezaji Kibu Denis kuangushwa mara tatu ndani ya eneo la hatari.

Hakutoa walau penalti moja, pamoja na matukio mengi ambayo viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba walilalamika kuwa walinyongwa na mwamuzi huyo.

Siku chache baadaye, waliojiita kama wazee wa Simba walijitokeza na kulalamika kuwa kulikuwa na mchezo mchafu, au mipango ovu dhidi ya timu yao iliyowashirikisha baadhi ya vigogo nchini, wakidai kumshinikiza mwamuzi huyo achezeshe kwa kuidhoofisha timu yao kwenye mchezo huo.

Wazee hao walidiriki hata kutoa mifano na kusema kama iliwezekana wanaweza kuwataja watu ambao walimshinikiza mwamuzi huyo.

Hata hivyo, wiki chache baadaye, Kamati ya Uendeshaji ya Bodi ya Ligi, ilikutana ambapo pamoja na mambo mengine ilisema suala la Kayoko na waamuzi wenzake, limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Waamuzi baada ya kuonekana kutoutendea haki mchezo huo wa dabi.

Ilikuwa ni mwanzoni mwa Desemba ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni, alipothibitisha kuwa shauri la mwamuzi huyo limepelekwa kwenye kamati hiyo kwa ajili ya kujadiliwa na wajumbe wa kamati hiyo na kutoa ushauri wa kitaalamu kabla ya kufanyiwa maamuzi.

Ni mwezi mmoja sasa, hatujasikia lolote kuhusu mwamuzi huyo, kitu ambacho kinatia kinatufanya tuhoji kuhusu maamuzi ya kamati hiyo na kama ameadhibiwa basi isiwe kimya kimya ili kuwafanya na wengine kuchukua tahadhari kwa kuongeza umakini wanapopewa dhamana ya kuchezesha mechi.

Kwa hali ya kawaida, kama mchezaji amefanya kosa lolote ambalo linahitaji Kamati ya Nidhamu na Hadhi za Wachezaji ikae, mchezaji anaendelea kucheza hadi maamuzi yatakapotolewa, kama atakuwa hajaadhibiwa kwa kadi ya njano au nyekundu ya uwanjani.

Na hata waamuzi wengine huwa hawasimamishwi, badala yake wanaendelea kuchezesha hadi pale kamati itakapotoka na maamuzi ndipo anapoanza kutumikia adhabu yake.

Kwa Kayoko sivyo, kwani hajaonekana tena kuchezesha mechi yoyote, huku suala lake likiwa kwenye Kamati ya Waamuzi.

Hii haimtendei haki hata yeye mwenyewe ambaye hajui hatma yake itakuwa nini na lini. Ni wakati sasa wa kamati husika kutoka na kuweka wazi kama ni kuadhibiwa itangaze na yeye kuanza kutumikia adhabu yake lakini pia kutoa fundisho kwa wengine wanaochezesha chini ya kiwango.

Kumuondoa kwenye ratiba kimya kimya, si sahihi kwani hakutatoa nafasi kwa wengine kutambua wakifanya makosa adhabu wataadhibiwa kwa kiwango gani, ili kuchukua tahadhari.

Lakini hivi kweli tumefika mahali sasa mambo yanakwenda kimya kimya mpaka wadau hatuelewi nini kinaendelea kwa suala la Kayoko? 

Je, wakubwa wanaogopa maswali? Wanaogopa kusema alikosea nini? Kuogoka kuongea suala hili au kutoa maamuzi kunawafanya wadau wa soka kufiriki na wao ni sehemu ya makosa yake. Labda sasa watuambie pia kuna kanuni ya kuadhibiwa kimyakimya? Ili nasi tuijue.