ZAMANI waliitwa wageni wa heshima, siku hizi wanaitwa wageni rasmi. Ni watu au viongozi wanaokuja uwanjani kwa ajili ya sababu maalum, ikiwamo kutoa zawadi na kukabidhi kombe.
Huu ni utamaduni wa tangu miaka ya nyuma, lakini ukiangalia kwa wenzetu ambao walioanzisha soka wameshaachana na hayo.
Ukiangalia ligi mbalimbali duniani Ulaya na Afrika, huwezi kukuta kuna mgeni rasmi kwa mechi kama ya ligi isikuwa ya kukabidhiwa kombe. Utawaona kwenye michuano kama fainali za AFCON, kufungua mashindano na kufunga. Hata Ulaya ni hivyo hivyo. Kwa sasa huwezi kuwaona wageni rasmi kwenye kila mchezo.
Hapa Tanzania utamaduni huo umeonekana kuendelea kwa kile kinachoonekana ni mazoea.
Kila mchezo uwe ni wa Ligi Kuu au Championship, basi utamwona mgeni rasmi, tena yoyote yule, ili mradi tu inawezekana mtu kidogo mwenye wadhifa wake kwenye taasisi, serikalini au chama cha soka.
Binafsi, naona kama utamaduni huu umepitwa na wakati, badala yake waache soka liendelee kuwa soka na mgeni rasmi awepo kwenye mashindano au matukio makubwa.
Kinachotakiwa hapa ni kwamba hata siku mashabiki wakisikia mgeni rasmi, kwenye mechi kubwa na muhimu na mara nyingi wanakuwa ni viongozi wakubwa basi wawe na hamu ya kuona tukio hilo, tofauti na sasa ambapo wageni rasmi wamekuwa wengi.
Kitendo cha kila mchezo kuwa na mgeni rasmi ambaye anaingia uwanjani kupiga picha na wachezaji pamoja na waamuzi wakati mwingine ndiko kunakosababisha baadhi ya wanasiasa kujiingiza moja kwa moja kwenye masuala ya soka ambapo Shirikisho la Mpira wa Miguu Dunia (FIFA), wameshakataa.
FIFA wameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa kutenganisha vitu hivyo, pamoja hata na kuwaengua askari polisi kulinda usalama ndani ya uwanja.
Ukiangalia askari kwa sasa kwenye michezo ya kimataifa wanalinda zaidi nje ya uwanja na ndani kuna watu maalum tu walioandaliwa na kupewa mafunzo kwa ajili hiyo.
FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wanaona mashabiki wanaokuwa uwanjani si wahalifu, bali ni wateja wao, hivyo hawahitaji nguvu iliyopitiliza, badala yake yeyote anayekwenda kinyume cha utaratibu, walinzi maalum wanajua jinsi gani ya kudili naye kwa namna ambayo wamefundishwa.
Mfano wa hili ni wale mabaunsa wa Al Ahli Tripoli ambao walikuwa wanawalinda wachezaji wa timu hiyo waliokuwa wakihofia kufanyiwa vurugu na mashabiki wa Simba kulipa kisasi cha kile kilichotokea Libya, walizuiwa kuingia uwanjani. Kwanza hawakuwa na tiketi, pili hawakutakiwa kwa sababu ya kutoleta taharuki na kuambiwa hata ndani ya uwanja kuna walinzi ambao watawalinda wachezaji hao na si wao. Na hii ni kwa sababu ilikuwa ni michuano inayosimamiwa na CAF. Sijui kama ingekuwa ni ligi ingekuwaje kama wangeingia nao uwanjani au vipi.
Hii inaonesha kuwa wenzetu, wamekuwa wakipiga hatua kila miaka inavyozidi kusonga mbele si kwenye maendeleo ya soka na miundombinu tu, lakini hata kwa maeneo mbalimbali, ikiwamo ulinzi, itifaki na vingine vinavyofanana na hivyo.
Ndiyo maana tunaona leo hawana mgeni rasmi, hadi pale kwenye ufunguzi wa michuano mikubwa na mechi ya fainali na wanaokwenda hapo ni viongozi wakubwa wa nchi na mashirikisho ya michezo.
Hapa kwetu hadi leo, mjumbe wa chama cha soka anakuwa mgeni rasmi wa mchezo. Shabiki akiruka kutaka kuingia uwanjani anakimbiliwa na askari na kupigwa virungu kama mwizi aliyepora simu.
Nadhani umefika wakati tuangalie wenzetu wanafanyaje, ili na sisi twende kutokana na mabadiliko. Isije tukawa tunakwenda sehemu ambayo wenzetu wanatoka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED