WIZARA ya Fedha na Mipango Zanzibar, wiki iliyopita ilieleza kuhusu kuchakaa noti ya Tanzania, kunakofanywa na baadhi ya wananchi, wanapokuwa kwenye sherehe mbalimbali za kijamii.
Wizara hiyo ilieleza kuwa kuchakaa kwa noti hizo, kunatokana na matumizi mabaya kwenye wimbi la sherehe za harusi nchini.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, alikaririwa akiyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi visiwani humo, wakati akijibu swali la mmoja wa wawakilishi aliyetaka kujua matumizi haramu ya noti hizo na hatua zinazochukuliwa kwa mtu anayebainika, anaidhalilisha na kushusha thamani noti hiyo.
Alichosema waziri ni sahihi kabisa, kuwa kuna watu wamekuwa na tabia ya kurusha kwa maharusi noti iwe sakafuni, ukumbini na kwingine kisha kukanyagwa.
Vilevile wako wanaoviringisha noti katika maumbo na kutumika kama mapambo na kuweka kwenye mwili wa mtu wenye jasho na kusababisha kuchakaa na kukosa hadhi yake stahiki.
Siyo hivyo tu, noti hizo pia zimekuwa zikihifadhiwa vibaya na baadhi ya wafanyabiashara wakiwamo wa mkaa na kusababisha kuchakaa kwa kukunjwa, visivyo na kuchafuka masizi kiasi cha kutokuwa na thamani kwa kuanza kuchanika.
Vilevile noti hizo zimekuwa zikichakaa kutokana na wafanyabiashara wa maji kuzihifadhi zikiwa zimelowa baada ya kupokea kutoka kwa wateja.
Mitaani kuna noti, ambazo ziko kwenye mzunguko wa biashara zimechakaa kutokana na wafanyabiashara kukosa umakini katika kuzihifadhi.
Kati ya noti hizo, zipo ambazo zimekatwa kwenye kona kwa madai kuwa ya kudhibiti kuibwa kwa njia ya mazingaombwe maarufu kama chuma ulete.
Ni ukweli usiopingika kuwa uchakavu huo wa noti, unaipotezea sifa fedha hiyo ya Tanzania, kwa kuwa ni moja ya tunu za taifa letu.
Kinachosikitisha kuwa, vitendo hivyo vinaendelea kukithiri nchini, licha ya kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), maofisa wake waandamzi na viongozi wa serikali wamekuwa wakikemea na kuitaka jamii kulinda tunu hiyo.
Jamii inatakiwa kuelewa kwa tabia hiyo ya kuharibu noti na sarafu inatakiwa kukomeshwa kwani ni dharau na dhihaka kwa Serikali.
Ieleweke kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ina kifungu kinachoainisha kuwa ni kosa la jinai kwa kutumia vifungu na kanuni za adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2002.
Hivyo, mwananchi atakayebainika akitenda kosa hilo iwe kwa bahati mbaya au makusudi akamatwe na kushtakiwa kwa kosa la jinai na kuhukumiwa kutumikia kifungo jela, ili kukomesha tabia hiyo ambayo imekuwa ikiota mizizi siku hadi siku.
Watanzania ieleweke kwamba serikali inatumia fedha nyingi, kwa ajili ya kuchapisha noti mpya na kutengeneza sarafu, hivyo ni jukumu letu kuisadia kupunguza gharama kwa kuokoa fedha ambazo zinatumia kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa yetu sote.
Miradi hiyo ya jamii ni pamoja na kusogeza huduma ya maji, umeme, elimu, afya na ujenzi wa barabara, madaraja na mingine mingi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED