Nafasi ya Yanga robo fainali michuano ya CAF hii hapa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:32 AM Dec 09 2024
Wachezaji wa Yanga
Picha: Mtandao
Wachezaji wa Yanga

KIPIGO cha mabao 2-0 ilichokipata Yanga juzi dhidi ya MC Alger ya Algeria, kimewafanya baadhi ya mashabiki wao kuanza kukata tamaa ya kupita hatika hatua ya makundi.

Baada ya mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Julai 5 jijini Algiers, mashabiki wengi waliokuwa wakiangalia kwenye televisheni na hata ukisoma kwenye mitandao ya kijamii, wanaonekana kukata tamaa kuwa inawezekana msimu huu timu yao isiweze kupita hatua ya makundi na kwenda robo fainali kama ilivyokuwa msimu uliopita, ilipotolewa hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, baada ya suluhu katika michezo yote miwili ya nyumbani na ugenini.

Sababu kubwa ni kipigo cha pili mfululizo ilichokipata kwenye michuano hiyo, cha kwanza ikikipata nyumbani dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, ikichapwa pia mabao 2-0.

Nadhani hawaoni mwanga tena mbele, kwani katika michezo hii, malengo makubwa ya timu zinazotaka kupita makundi ni kushinda mechi zote tatu za nyumbani kwanza. Inawezekana kabisa pointi hizo zinakufanya kupita kwa kushika nafasi ya pili, lakini pia zipo timu zinashinda ugenini au kupata hata pointi moja.

Mfano Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema lengo ni kupata pointi 10, ambazo mpango wake ni kuzipata tisa nyumbani na moja kuipata katika mechi tatu za ugenini ambazo zitamwezesha kusonga mbele.

Haya ndiyo mahesabu ya michuano hii ya kimataifa kwa timu ambazo ziko 'siriasi' hasa.

Yanga imepoteza mechi moja nyumbani na moja ugenini. Kwa maana hiyo, mahesabu yake sasa ni kushinda michezo yote mwili ya nyumbani ili kupata pointi sita kwanza.

Halafu ishinde mechi moja ugenini na moja sare katika michezo miwili ya ugenini iliyobaki.

Kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga wanaona kama itakuwa ngumu kutokana na mwenendo wao kwa siku za karibuni hata kwenye michezo ya Ligi Kuu.

Niwatoe wasiwasi wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa wasikate tamaa timu hiyo inaweza kuvuka hatua hii kama mikakati thabiti itapangwa.

Wasiwasi ni kwamba wanachama na mashabiki wa Yanga wanaweza wasijitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenda kuisapoti timu yao, kitu ambacho hawatakiwi kufanya hivyo kwani nafasi bado wanayo ya kusonga mbele.

Mara nyingi hawana tabia ya kwenda kujazana uwanjani kama timu yao inafanya vibaya. Hii inaweza kufifisha juhudi za viongozi na wachezaji kutinga hatua ya robo fainali.

Kinachotakiwa kwa wanachama na mashabiki wa Yanga, haijalishi timu inapitia kipindi kigumu liasi gani, lakini inatakiwa kujazana uwanjani ili kuipa nguvu.

Ikumbukwe kuwa Simba ilipitia kipindi kigumu kama hicho, mfano tu msimu uliopita, ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, suluhu ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, baadaye ikafungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.

Hapa utaona kuwa kwenye michezo mitatu ilikuwa haijashinda hata mchezo mmoja, lakini ikapambana na kushinda mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Wydad Casablanca, kabla ya kulazimishwa suluhu kwa mara nyingine dhidi ya Asec Mimosas ugenini.

Hii inaonesha kuwa Simba ilipita kwenye njia ngumu mno, kiasi kwamba mechi mbili za mwisho ililazimika kushinda zote, ikaifunga Jwaneng Galaxy mabao 6-0 na kutinga hatua hiyo.

Misimu mwili iliyopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo, ilionekana kama imeshatolewa kwenye kinyang'anyiro cha kutinga robo fainali kwa kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi, lakini ilishinda michezo miwili mfululizo dhidi ya Vipers ya Uganda na kurejesha matumaini, kabla ya mchezo wa mwisho kuikandamiza Huroya mabao 7-0, ikatinga kwa kishindo robo fainali.

Mifano hii ni kuonesha kuwa Yanga kama itakaa chini na kupiga hesabu zake vizuri, kuandaa mikakati ya ndani ya uwanja ya kiufundi ikichanganya na rasilimali watu ambao ni mashabiki wake kwa kuwahamasisha kujazana uwanjani kwenye kuipa sapoti, kama ilivyokuwa ikifanya Simba huko nyuma, ikipita mara kwa mara katika mazingira magumu, basi hakuna kitakachoshindikana kwa kutinga robo fainali.