MABADILIKO ya matumizi ya teknolojia ya mawasiliano duniani yameleta mafanikio na athari kutokana na watu wanavyoitumia teknolojia hiyo.
Mafanikio yaliyopatikana ni watu kupata fursa nyingi za kujifunza kupitia mitandao hasa inapotumika vizuri na wengine kutengeneza ajira ambazo zinawapatia vipato.
Vile vile, matumizi hayo yalisaidia kipindi ambacho dunia ilikumbwa na janga la Uviko na kusababisha wafanyakazi kuathirika na baadhi yao kupunguzwa kazi huku wengine wakilazimika kufanyakazi zao wakiwa nyumbani.
Teknolojia hiyo pia imesaidia masomo na mikutano kufanyika mitandaoni badala ya kukutana uso kwa uso na kuokoa gharama za watu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Hayo ndiyo matumizi mazuri ya teknolojia ambayo yanaleta tija kwa watu na nchi pia.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaitumia vibaya teknolojia hiyo kwa kurusha vitu vinavyozua taharuki na kuchafua watu wengine.
Teknolojia hiyo pia inatumiwa vibaya na baadhi ya watu wanaofanya uhalifu kwa kuingia kwenye akaunti za watu na kuiba fedha kimtandao na watu wengi wamelizwa kwa njia hiyo.
Kuna mambo mengi yanayotokea katika kipindi hiki huku wahalifu wakitafuta mbinu mbalimbali za kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko hayo.
Dunia kwenda na mabadiliko ya teknolojia ni kurahisisha kazi na kupunguza muda unaotumika kwa binadamu kuifanya kazi hiyo.
Pia wapo wanaotumia picha za matukio ya zamani na kuzitengeneza ili mradi kuwachafua watu na kuwaharibia wasifu wao. Teknolojia hii isitumike kuharibu badala yake itumike kujifunza mambo yenye maendeleo kwa faida yao na taifa.
Miaka ya nyuma sehemu zenye huduma muhimu kama ulipaji wa bili za umeme, maji na benki, mtu ilibidi aende kwenye ofisi hizo hali iliyokuwa ikisababisha msongamano mkubwa wa watu.
Sasa hivi hata ukiwa nje ya nchi unaweza kufanya miamala na kulipia bili zako kwa wakati.
Kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ilikuwa inachukua muda kumtumia ndugu yake pesa, lakini kwa sasa teknolojia imerahisisha.
Lakini, teknolojia hiyo imeingiliwa na kutumika vibaya kwa baadhi ya wahalifu kwenye sekta ya fedha kwa kuwaibia watumiaji na kuwafanya waogope kuitumia.
Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imeeleza wazi kuwa inaendeleza jitihada za kupambana na kudhibiti uhalifu mitandaoni, ikiwamo huduma za kifedha kutokana na kuongezeka mifumo mipya ya mawasiliano ya teknolojia.
Inapokuja teknolojia mpya ni muhimu ikatumika vizuri ili kunufaisha watu na kuondoa ugumu uliokuwapo mwanzo.
Kwa nchini Tanzania, wafanyabiashara, wajasiriamali wamerahisishiwa kazi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ambapo kwa sasa wanaweza kutuma pesa nje ya nchi na kuletewa bidhaa wanazotaka badala ya kusafiri hali inayowapunguzia gharama.
Katika matumizi ya teknolojia hii pia kunahitajika uaminifu wa hali ya juu ndio maana hata TCRA ikiwa ni mdhibiti wa matumizi mabaya ya mawasiliano imekuwa ikiingilia kati kila inapoona mambo hayaendi sawa.
Kuna wanaotumia teknolojia hiyo pia kwa malengo mabaya ya kuwachafua watu wengine kwenye mitandao.
Hali hiyo imekuwa ikishamiri kwenye mitandao ya kijamii kiasi cha kuharibu hali ya hewa na wengine wanaochafuliwa huathirika kisaikolojia.
Viongozi wa juu wanapokuwa kwenye majukwaa wamekuwa wakikemea tabia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa kama isipodhibitiwa itarudisha nyuma maendeleo.
Duniani mabadiliko ya kiteknolojia hayawezi kuepukika, hivyo ni muhimu wadhibiti wa uhalifu mitandaoni kuwa makini kudhibiti hali hiyo ili kuepuka matumizi mabaya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED