WANANCHI katika maeneo mbalimbali nchini, walijitokeza kupiga kura kuchagua viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji. Upigaji kura huo ulifanyika baada ya kukamilika kwa mchakato wa kujiandikisha na kufanya kampeni kwa vyama vilivyosimamisha wagombea katika nafasi za wenyeviti, wajumbe wa kamati mchanganyiko na makundi ya wanawake, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa maeneo ya vijijini.
Kama ilivyofanyika hamasa kubwa kwa wananchi hao wakati wa kampeni huku Rais Samia Suluhu Hassan akikoleza moto kwa wananchi kujitokeza kutumia haki yao ya kidemokrasia, wananchi walifika kwa wiki katika vito vya kupigia kura kwa wakati, katika baadhi ya maeneo mkoani Dar es Salaam, wananchi walifika kabla ya muda uliopangwa kwa vituo kufunguliwa, yaani saa 2:00 asubuhi.
Pamoja na kuwahi kufika vituoni mapema ili kupiga kura na hatimaye kwenda kwenye majukumu yao, baadhi ya wananchi wasishindwa kutekeleza jukumu hilo la kidemokrasia baada ya kukuta majina yao hayamo kwenye karatasi zilizobandikwa.
Pia wengine walihangaika kupata majina yao kwa kuwa hayakubandikwa kwa alfabeti kama ilivyozoeleka kwenye uchaguzi uliopita. Walipohoji kwa nini hali haikuwa kama wakati uliopita baadhi ya wasimamizi kwenye vituo hivyo walijibu kwamba majina yamebandikwa kama ilivyokuwa kwenye tarehe za uandikishaji, hivyo kuwataka wapigakura kwenye milango mbalimbali ya maeneo ya kupigia kura ili kuangalia majina yao.
Licha ya kuambiwa hivyo, baadhi ya wananchi waliofika mapema kwenye vituo walihangaika kutafuta majina yao bila mafanikio, hivyo kuamua kuondoka bila kupiga kura. Wananchi hao walishutumu utaratibu mbovu uliowekwa ambao walidai umewakosesha haki yao ya kidemokrasia huku wengine wakisema inawezekana ni njama ya kuwafanya wengine kukosa kupiga kura.
Kadhalika, katika baadhi ya vituo, mtu baada ya kuliona jina lake, aliruhusiwa kupiga kura bila wasimamizi na mawakala wa vyama waliokuwa katika vyumba vya kupigia kura kuhakiki jina na kujiridhisha kama mhusika ndiye. Hatua hiyo ingeweza kusababisha mtu yeyote akafanya udanganyifu na kupewa karatasi ya kura na kupiga hatimaye kuondoka zake.
Aidha, katika baadhi ya maeneo, zilitolewa taarifa mbalimbali kuwa baadhi ya wagombea majina yao hayakuwamo kwenye makaratasi ya kupigia kura licha ya kwamba walipishwa kuwania nafasi husika.
Kasoro hizo zilizoainishwa ni ndogo na zinasababishwa na wasimamizi lakini serikali na chama tawala ndivyo vinatwishwa mzigo wa lawama hali inayotia doa mchakato mzima wa uchaguzi na kwenda kinyume cha maagizo ya Rais Samia kuwa kila mtendaji kwenye mchakato huo atende haki.
Kwa ujumla, yako baadhi ya makosa ambayo yanaonekana dhahiri kuwa ni uzembe wa wasimamizi, hivyo mamlaka zilizopewa dhamama ya kusimamia kazi hiyo kuchukua hatua ili kuepusha malalamiko yanayoweza kuufanya mchakato kutokuwa huru na haki.
Ni vyema serikali kupitia Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hasa wasimamizi wa uchaguzi ngazi za halmashauri, kuchukua hatua dhidi ya wale wote watakaobainika kwa njia yoyote wamesababisha doa katika uchaguzi huo ambao ndilo chimbuko la demokrasia na utawala bora.
Haiwezekani serikali ikatumia mabilioni ya shilingi kuandaa uchaguzi huo lakini watu wachache wautie doa kwa maslahi ya mtu au kikundi cha watu wachache. Watu wa namna hiyo wachukuliwe hatua kwa kuwa kuharibu uchaguzi au kuutia doa lolote ni sawa na uhujumu uchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED