LEO Yanga wana karata moja muhimu katika harakati zao za kutaka kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapokuwa wageni wa TP Mazembe katika mchezo wa kundi A wa michuano hiyo.
Ni karata muhimu kutokana na ukweli kuwa mchezo huo umebeba matumaini ya wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya vilabu barani Afrika.
Endapo Yanga ambayo imepoteza michezo yake miwili iliyopita, ikipoteza na mchezo wa leo utakaochezwa saa 10 jioni, itakuwa imejisafishia njia ya kuondolewa kwenye michuano hiyo.
Mpaka sasa ndio timu pekee kwenye kundi lake ikiwa haina pointi yoyote licha ya kucheza michezo miwili sawa na timu nyingine kwenye kundi hilo.
Matumaini pekee ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo yanabaki kwa wachezaji wa timu hiyo ambao ndio wanakazi kubwa ya kufanya ndani ya dakika 90 za mchezo huo.
Tunaamini Yanga wana timu nzuri na wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kusakata soka, na wanaweza wakatoa matokeo yoyote ndani ya dakika 90 za mchezo.
Hata hivyo wachezaji lazima watambue umuhimu wa mchezo huu wa leo kwa ajili ya mustakabali wa malengo yao ya kutaka kucheza kwa mara ya pili mfululizo hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Lakini pia bila ubishi ili kuweza kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huu, ni lazima wachezaji wavuje jasho uwanjani na kujitoa muda wote wa mchezo kusaka alama tatu muhimu.
Kwenye soka hakuna kinachoshindikana, kama wachezaji wa Yanga watafuata maelekezo ya kocha wao na kuonesha juhudi muda wote wa mchezo, uwezekano wa kuvuna alama tatu upo.
Hakuna ubishi kuwa mchezo wa leo ni mgumu kwa pande zote, ugumu huo unatokana na uhitaji wa pointi tatu kwa kila timu kuweza kuweka hai matumaini yao ya kusonga mbele.
Yanga ambayo haina pointi yoyote, wanakutana na TP Mazembe yenye pointi moja waliyoivuna kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya MC Alger huku timu zote zikipoteza kwenye michezo yao ya pili Yanga wakifungwa na Alger mabao 2-0 huku Mazembe wakikumbana na kipigo kutoka kwa Al Hilal.
Tunaishauri Yanga kuingia uwanjani kwa tahadhari wakisahau matokeo waliyoyapata mwaka jana dhidi ya wapinzani wao hao kwenye kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga walipata ushindi nyumbani na ugenini.
Kama wachezaji wataamua kupambana kweli na kila mmoja kucheza kwenye kiwango chake cha juu, Yanga wana nafasi ya kupata ushindi kwenye mchezo huo.
Kwenye soka hakuna kinachoshindikana, ndani ya dakika 90 ni kupambana na kuwa makini kwa kila nafasi watakayoipata, tunaamini kutokana na ugumu wa mchezo huo kwa kila timu, hakutakuwa na nafasi nyingi za wazi za kuweza kufunga.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga wanapaswa kuwa makini na kila nafasi watakayoipata,watumie nafasi hizo kupachika mabao na kuihakikishia timu ushindi.
Nipashe tunawatakia kila la heri Yanga tukiamini uwezo wa kushinda mchezo wa leo wanao na kuweka hai matumaini ya kuwa timu moja wapo watakaoingia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED