KAZI ya kuendesha pikipiki ambazo ni maarufu kama 'bodaboda', ni biashara pia ni ajira kama zilivyo ajira nyingine halali zinazowaingizia watu vipato vya kuendeshea maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo, baadhi ya vijana ambao wameingia katika ajira hiyo ni kama wamekuwa wazito kuelewa umuhimu wa ajira hiyo na kuiheshimu ili iweze kuwanufaisha wao na familia zao.
Kwanini? Kwa sababu kila uchao wamekuwa wakiibuka na mitindo ambayo ni hatari kwa maisha yao, aidha kwa kuelewa au kutoelewa madhara ya kile wanachokifanya wawapo barabarani.
Wamekuja na mtindo ambao inawezekana wanauona ni wa kawaida, lakini ukweli ni kwamba unaweza kuwasababishia madhara makubwa iwapo wataendelea nao au wasipodhibitiwa.
Mtindo wenyewe ni wa kutawala barabara na kuendesha bodaboda kwa fujo bila tahadhari huku wakifanya vituko vya kuachia usukani, wanapokuwa katika msafara wa kusindikiza mwenzao aliyefariki dunia au mambo yanayofanana na hayo.
Wakati mwingine, baadhi yao hubebana hata wanne kwenye bodaboda moja, wengine wakiendesha huku wamesimama. Yaani hufanya kila aina ya vituko barabarani, ambavyo ni hatari kwa usalama wao.
Vilevile, kuna kero ambayo madereva hao wanachangia ya kutawala pande zote za barabara kwa muda na kusababisha watu wengine washindwe kuitumia kana kwamba ni mali yao.
Sijui mikoa mingine, lakini kwa Dar es Salaam imekuwa kama jambo la kawaida kusikia honi nyingi zikipigwa pale wanapokuwa wakisindikiza msafara wa msiba wa mwenzao huku wametanda barabara yote.
Kwa ujumla ni kwamba wanajiweka katika mazingira ya kuhatarisha maisha yao na pia wanasababisha kero kwa watumiaji wengine wa barabara. Hivyo, ingependeza kama watadhibitiwa.
Nilidhani kwamba mwenzao anapopoteza maisha, ni wakati mwafaka kwao kutafakari na kuchukua tahadhari zaidi wawapo barabarani, lakini ajabu wanaendelea kujiweka katika mazingira hatarishi.
Yawezekana aliyefariki atakuwa amesababishiwa ajali au amesababisha mwenyewe, lakini bado wanapaswa kutambua kuwa umakini unahitajika wawapo barabarani, sio kujiendea wanavyotaka.
Udereva wa bodaboda ni ajira ambayo imesaidia vijana kuacha kushinda vijiweni, lakini bahati mbaya baadhi yao wanashindwa kuheshimu ajira hiyo na kusababisha ionekane kama kazi ya kihuni.
Kutoheshimu ajira hiyo kunachangia kuwapo kwa ajali nyingi zinazogharimu maisha yao na ya abiria, kwani baadhi yao huwa wanatuhumiwa kujihusisha na ulevi wa pombe wawapo kazini.
Inaelezwa kuwa ajali za bodanoda bado ni tishio, kwani Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI), inasema inapokea wagonjwa takriban 700 kwa mwezi huku asilimia 60 ya wagonjwa hao wakitokana na ajali za bodaboda.
Hayo ni kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa MOI), Dk.Lemeri Mchome, alipoitoa wakati fulani akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vya tiba, kutoka kwa wadau wa afya.
Kwa taarifa hiyo, ni wazi kwamba kuna ombwe kwa madereva wa bodaboda la kutokuwa makini wawapo katika ajira hiyo na kujisababishia madhara au kuwasababishia abiria wao.
Jambo ambalo angalau sasa wanaliheshimu, ni kutojichukulia sheria mkononi kama zamani walipokuwa wakiona mwenzao amegongwa na gari wanavamia na kutembeza kipigo bila kujua chanzo cha ajali.
Lakini wizi, kutotii sheria za usalama barabarani kama kutovaa kofia ngumu, kulewa, kubeba abiria zaidi ya mmoja, kuvuka katika makutano ya barabara bila kuruhusiwa na taa, hayo yanaendelea kama kawaida.
Ukweli ni kwamba bodaboda zimeongeza ajira, kurahisisha usafiri maeneo ya mijini na vijijini, lakini tatizo ni wahusika kushindwa kuheshimu kazi hiyo na kusababisha wao kama nguvukazi ya taifa kupotea bure.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED