Undugu huu ni tishio abiria

By Tuntule Swebe , Nipashe
Published at 01:22 PM Dec 18 2024
Undugu huu ni tishio abiria
Picha:Mtandao
Undugu huu ni tishio abiria

MAKONDAKTA wa daladala inavyoonekana ni marafiki wakubwa wa wapigadebe waliopo kwenye vituo mbalimbali vya mabasi.

Ni kutokana na ukweli  kwamba wengi wa makondakta hao ni zao au  wametoka kwenye kundi hilo.
 
 Ushirika huo umejenga  urafiki kati ya makundi hayo mawili na hupeana kazi ya kupiga debe, kwa ajili ya kujaza abiria ndani ya daladala kwenye vituo vya mabasi mikoani na majijini  na kupewa ujira wa shilingi 200 hadi 500.
 
 Hata hivyo, baadhi ya wapigadebe wanatuhumiwa kujihusisha na tabia ya kuwachomolea fedha abiria na inawezekana hata vitendo hivyo hufanyika huku makondakta wakijua.
 
 Kuwanyamazia wezi hao kunatokana na ukweli kwamba ni marafiki zao wa karibu wanaopeana kazi ili mkono uende kinywani. Lakini ni vyema wakatambua kuwa wanaharibu kazi yao.
 
 Mtindo huo si mpya bali ni wa muda mrefu, lakini sina budi kukumbusha kuwa inatosha kuwalea watu wa aina hiyo kwa kuwapa kiasi hicho cha fedha ambacho kimsingi hakitoshi kuendesha maisha.
 
 Jambo la muhimu ni kusaidiana kutafuta kazi halali ambazo zitawasaidia kuendesha maisha badala ya kujificha chini ya mwamvuli wa upigadebe huku wakiwaibia abiria ndani ya daladala.
 
 Inasikitisha kuona kijana mwenye nguvu zake anashinda katika kituo cha daladala na kufanya kazi ya kuibia abiria badala ya kutumia nguvu hizo kufanya kazi halali kwa ajili ya maisha ya baadaye.
 
 Muda ambao abiria wamekuwa wakiibiwa ni asubuhi wanapokwenda kazini na hata jioni wanaporejea majumbani, kutokana na kwamba ndio wakati ambao daladala nyingi huwa zimejaa abiria.
 
 Kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo ambavyo pia uhusisha vibaka wengine, ingekuwa ni vyema sasa kazi ya ukondakta ikawa ni kazi rasmi inayoheshimiwa badala ya kuwa na watu wa ziada.
 
 Yaani madereva na makondakta waajiriwe ili kuondoa sintofahamu hiyo, kwani wakiwa katika ajira, haitakuwa rahisi kuruhusu wapigadebe kuwasaidia kufanya kazi ya kuita abiria.
 
 Kuwapo kwa wapigadebe kunatokana na uholela wa kazi hiyo, lakini kama wahusika wataajiriwa, itakuwa ni rahisi kufanya kazi yao kwa umakini bila kuruhusu wapigadebe kuwasogelea.
 
 Uholela wa kazi hiyo umesababisha karibu vituo vyote vya daladala hasa jijini Dar es Salaam kujaa wapigadebe ambao wanajificha chini ya mwamvuli wa upigadebe lakini wakijihusisha pia na wizi.
 
 Ninaamini katika mazingira hayo, itabidi wapigadebe watafute kazi nyingine halali ya kufanya badala ya kuhangaika na shughuli ambazo hazina manufaa yao ya baadaye.
 
 Sio vibaya wakajiunga katika vikundi na kupata mkopo wa fedha zitakazowawezesha kuanzisha biashara ili waweze kujikimu kimaisha kuliko kuhangaika na vitu ambavyo havina manufaa kwao.
 
 Vilevile, umefika pia wakati wa kuacha mtindo wa kurundika abiria ndani ya daladala kama mizigo, kitendo ambacho ni hatari kwani kinaweza kusababisha wakaambukizana magonjwa.
 
 Ingependeza kama askari wa kikosi cha usalama barabarani wakalisimamia hilo, ili kila daladala ibebe abiria na kuwaachia nafasi ya kupumua hata kama kuna changamoto ya usafiri.
 
 Ninajua kuwa katika jiji la Dar es Salaam, kuna changamoto ya ukosefu wa usafiri wa kutosha wa daladala, lakini hilo lisiwe kigezo cha kurundika abiria ndani kupita kiasi.
 
 Ikumbukwe kuwa vijana ndio taifa la kesho linalotegemewa kuisaidia nchi, hivyo wasiachwe katika mazingira hayo ambayo yatawafanya wawe taifa la kesho lisilo na umuhimu ndani ya jamii.
 
 Zipo njia mbalimbali nilizotaja za kuwasaidia wapigadebe hao, lakini pia makondakta wenyewe wajaribu kupunguza urafiki na kundi hilo ili kulinda heshima ya kazi yao mbele ya abiria.