Dk. Manguruwe aandika barua kwa DPP kukiri kosa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:20 AM Dec 19 2024
Dk. Manguruwe aandika barua kwa DPP kukiri kosa.
Picha:Iman Nathanael
Dk. Manguruwe aandika barua kwa DPP kukiri kosa.

MKURUGENZI mwanzilishi wa Vanilla International Limited, Simon Mkondya, maarufu Dk. Manguruwe, anayeshtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi, amemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kuingia makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining).

Dk. Manguruwe pamoja na Rweyemamu John ambaye ni mkaguzi wa kampuni hiyo, wanashtakiwa kwa mashtaka 28 yakiwamo ya kujipatia zaidi ya Sh. milioni 90 kwa udanganyifu na utakatishaji, kwa kununua viwanja tisa eneo la Idunda mkoani Njombe. 

Wakili wa Serikali, Winiwa Kashala, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Anna Magutu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na pia upelelezi bado haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa. 

Hata hivyo, alidai kuwa Dk. Manguruwe ameandika barua ya ‘plea bargaining’ lakini hawajakubaliana na ombi hilo hadi upelelezi wa kesi hiyo ukamilike. 

Hakimu Magutu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 2, 2025 kwa kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi itakapofikia. Dk. Manguruwe anaendelea kusota rumande kwa sababu anashtakiwa kutakatisha Sh. milioni 90. 

Mshtakiwa wa pili aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 45. 

Ilidaiwa kwamba washtakiwa hao walitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam. 

Ilidaiwa kwamba mashtaka 19 ni ya kufanya biashara ya upatu. Katika  kipindi hicho Mkondya akiwa mkurugenzi na John akiwa mfanyakazi wa kampuni hiyo, wanadaiwa kufanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu kulingana na kiasi cha fedha watakazotoa. 

Ilidaiwa kwamba washtakiwa hao walijipatia kiasi cha jumla ya Sh. milioni 92.2 kutoka kwa watu 19 tofauti na watu hao walitoa kiasi tofauti cha fedha na  aliwaahidi watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa. 

Iliendelea kudaiwa kwamba, mashtaka tisa ni ya utakatishaji yanayomkabili Mkondya pekee na kwamba kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa kama mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia viwanja tisa kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya upatu.