MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imeteketeza kilogramu 614.12 za dawa za kulevya katika kiwanda cha saruji cha Twiga, kilichopo Wazo, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hilo leo, Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo, amesema kati ya dawa zilizoteketezwa, kilo 601.87 ni methamphetamine na kilo 12.25 ni heroin.
Amesema dawa hizo zilikuwa zinashikiliwa kama vielelezo na Mahakama za Hakimu Mkazi Kibaha na Mahakama za Hakimu Mkazi Kisutu, ziliamuru uteketezaji wake kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo, wakati kesi husika ikiendelea.
"Uteketezaji wa dawa hizi unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya Mwaka 2015 pamoja na kanuni zake.
“Sheria hii inaruhusu uteketezaji wa dawa hizi kufanyika kabla, wakati au baada ya shauri kumalizika mahakamani," ameeleza Kamishna Lyimo.Amefafanua kuwa uteketezaji huo unafanywa kwa njia zinazozingatia usalama wa afya ya watu na utunzaji wa mazingira, huku ukisimamiwa na wadau mbalimbali waliotajwa kisheria.
Amebainisha kuwa Desemba mwaka huu, pekee, mamlaka imefanikiwa kuteketeza ekari 12 za mashamba ya bangi katika mkoa wa Tabora pamoja na kilo 398.105 za dawa mbalimbali mkoani Mtwara. Pia, mamlaka inatarajia kuteketeza kilo 126.21 za mirungi mkoani Arusha katika siku chache zijazo.
"Tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa dawa hizi haramu zinadhibitiwa kwa ustawi wa jamii yetu," ameongeza.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED