Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TMNC) linaratibu na kuendesha mtihani wa usajili wa leseni kwa watahiniwa 5,147, unaotarajiwa kufanyika Desemba 20 mwaka huu.
Mtihani huo utafanyika katika vituo saba na unahusisha wahitimu wa kada za uuguzi na ukunga kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mtihani huu unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010, kifungu namba 6(o) na 15(1)(a).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Msajili wa Baraza hilo, Agnes Mtawa, amesema lengo la mtihani huo ni kupima umahiri wa wanataaluma kabla ya kusajiliwa na kupewa kibali cha kutoa huduma kwa jamii.
Mtawa amesema watahiniwa hao 5,147 wamekidhi vigezo vya kufanya mtihani huo. Wanajumuisha ngazi mbalimbali za elimu: Astashahada (86), Stashahada (4,498), Stashahada ya Uuguzi (537), Shahada ya Ukunga (11), na Shahada ya Uuguzi katika utoaji dawa za usingizi na ganzi (15).
Ameorodhesha vituo vya mitihani kuwa ni:
Kwa mara ya kwanza, Baraza litatoa mtihani kwa wauguzi wataalamu wa utoaji dawa za usingizi na ganzi, ambao pia utajumuisha mtihani wa vitendo ili kupima umahiri wao katika huduma hiyo maalum.
Mtawa ametoa wito kwa watahiniwa kuhakikisha wanawasili kwenye vituo vyao siku moja kabla ya mtihani, wakiwa na vifaa muhimu na katika mavazi nadhifu.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Taaluma ya Uuguzi nchini, Happy Masenga, amewahimiza watahiniwa kuzingatia mabadiliko na kanuni za taaluma. Amesema mtahiniwa ambaye hatofanya mtihani huo hatasajiliwa na Baraza hilo na hatakuwa na kibali cha kufanya kazi.
Aidha, Masenga amewakumbusha viongozi wa afya kuhakikisha kuwa wauguzi na wakunga wote katika maeneo yao wana leseni halali, ili kuhakikisha huduma bora kwa jamii.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED