WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amewasisitiza vijana kutumia fursa ya majukwaa mbalimbali katika kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yatakayojumuishwa kwenye dira hiyo.
Ridhiwani ameyasema hayo leo mkoani Dar es Salaam wakati wa kongamano la vijana kuhusu uhakiki wa rasimu ya dira ya taifa ya maendeleo 2050.
Amesema serikali imeendelea kuwekeza katika maeneo mengi kama elimu, afya, na mambo yote ya ustawi wa jamii ili kuhakikisha vijana wananufaika.
"Nini maoni yenu vijana juu ya haya yanayofanyika leo kwa ajili ya kesho yetu, hili ndilo jambo tunalolitaka kulisikia kutoka kwenu ili tuweze kuona kipi cha kufanya," amesema Ridhiwani.
Ameongeza kuwa katika maoni mbalimbali yaliyotolewa na vijana, wengi wamezungumzia kwa ukubwa uhitaji wa kuimarisha afya ili nguvu kazi ya vijana ipate kuimarishwa na kuwa na tija kwao na kwa taifa kwa ujumla kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.
"Maeneo ambayo yamefanyiwa kazi katika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Mwaka 2007 ambayo yamefanyiwa marejeo mwaka 2024, ni pamoja na elimu na ujuzi, uvumbuzi na ubunifu, na mapinduzi ya kidijiti. Mambo haya yanaweza kuchambuliwa katika kipindi kama hiki cha kutoa maoni ya dira", amesema Ridhiwani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED