MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amechukua fomu kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho huku akiwajibu watu wanaokosoa uamuzi wake na kusema jambo hilo si la ajabu na kuwahoji walitaka achukue nani.
Akizungumza jana asubuhi nyumbani kwake Tegeta, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuchukua fomu, Lissu alisema siyo ajabu yeye kugombea nafasi hiyo na wala kupambana na mwenyekiti wake (Mbowe).
Katika mahojiano hayo na kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, Lissu alisema kitu ambacho watu wanakiona cha ajabu ni yeye kuwa Makamu Mwenyekiti na kutangaza kuchukua fomu ya uenyekiti CHADEMA.
“Sasa mlitaka achukue nani kama siyo Makamu Mwenyekiti? Nani ndiye aliyeandikiwa kuchukua na nani asichukue? Kinachoonekana cha ajabu ni hicho tu,” alisema.
“Kinachoonekana cha ajabu ni hicho tu na Mwenyekiti mwenyewe hajasema kama anagombea. Kelele yote ni kwa sababu mimi nimesema wakati mwenyekiti hajasema. Msingi wa kelele hizo kisheria na katiba ya chama hakuna na hata nikigombea, nisipochaguliwa nitakuwa sijawahi kuwa mwenyekiti wa chama, nikichaguliwa nitakuwa mwenyekiti wa nne CHADEMA,” aliongeza.
Lissu alisema hana ugomvi wala vita na Mbowe au viongozi wengine wakuu CHADEMA ndiyo maana baada ya kutangaza nia yake, waliketi pamoja katika kikao cha kamati kuu ya chama hicho.
Kuhusu madai ya rafu zilizowahi kutokea wakati wa uchaguzi wa kanda wa chama hicho endapo kama hafikirii zitatokea katika uchaguzi wa Januari, Lissu alisema kama zilitokea ngazi ya chini zinaweza kutokea ngazi za juu.
“Watu wanasema kwa nini unasema haya hadharani. Yasiposemwa hadharani yasemewe wapi? Tuna mwongozo dhidi ya rushwa ndani ya chama ambao umeingiza makatazo yote ya rushwa ya uchaguzi yaliyoko katika sheria za nchi,” alisema.
KUHAMA CHADEMA
Kuhusu endapo ikatokea katika uchaguzi huo akashindwa kwa hila atafanya nini, Lissu alisema: “Kwanza niweke wazi maana yake kuna vimaneno maneno huyu anatengeneza namna ya kuhama. Kwanza, hahami mtu.”
Lissu alisema yeye ni mwanamageuzi na kudai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), hakijawahi kuwa chama cha mageuzi na hakitakaa kiwe. Alisema ana miaka 20 ndani ya CHADEMA tangu alipojiunga, kwamba kuna damu, jasho na fedha yake kidogo.
Lissu alisisitiza kwamba kama kuna hila, udanganyifu au kuingiliwa hayo ni mambo ambayo hajawahi kuyanyamazia na kuahidi hatofanya hivyo.
Alipoulizwa kama anadhani mfumo utafurahia awe mwenyekiti, Lissu alisema: “Sina shaka hata kidogo kwamba mfumo hauwezi. Kama mfumo una maana hawa watawala ambao wamekuwapo madarakani ambao wamekuwapo zama zote hizi, hawawezi kufurahi mimi kuwa madarakani. Kwa taarifa yako wameshaanza”.
Katika mahojiano hayo, Lissu pia alielezea kuhusu andiko lake aliloliweka katika akaunti ya X juzi inayozungumzia watu wasiojulikana wanaotaka kumdhuru ili wamsingizie mwenyekiti wake, Mbowe.
“Juzi kuna mtu mmoja alinitafuta naomba nihifadhi jina lake, tangu nilipotangaza habari hii (kugombea uenyekiti). Alipiga simu zaidi ya mara 10, ninafahamiana naye ni mtu mkubwa sana na wa heshima sana.
“Si mtu wa kuzusha maneno, si kiongozi serikali, lakini ni mtu mkubwa sana katika nchi hii. Jana (juzi) nikaangalia simu yangu nikakuta miss call nyingi sana za huyu baba.
“Nikamtafuta mawasiliano hayakuwa mazuri alikuwa safarini, lakini jioni tukapata mawasiliano mazuri akanipigia akaniambia ‘nimekutafuta sana jana na nimekutafuta kukuambia tafadhali ongeza ulinzi’, alisema na kusisitiza waliwasiliana kwa whatsApp.
Lissu alisema baada ya taarifa hiyo, alipomuuliza mtu huyo kama anamruhusu kutangaza suala hilo alimruhusu, ndipo alipoamua ku-tweet.
“Sijazungumza na Mbowe lakini nime-tweet ila nitazungumza naye. Hatua ya kwanza niliyofanya ni kupiga kelele kwa sababu hata mara ya kwanza nilifanya hivyo, lakini haikupita muda,” alisema.
ACHUKUA FOMU
Jana asubuhi, Lissu akiwa na wasaidizi wake alifika ofisi za CHADEMA zilizoko Mikocheni, Dar es Salaam na kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Lissu alisema endapo atachaguliwa atataka Tanzania ambayo watu wanaopenda haki.
“Kwa kuwa wenye haki wakiwa na mamlaka watu hufurahi na waovu wakitawala, watu huugua. Nataka uenyekiti wangu uwe ni kwa ajili ya kuhakikisha Tanzania yenye haki itakayoinua taifa letu na kufanya watu wetu wafurahi,” alisema.
Lissu alisema licha ya kujitokeza kwa kundi la wafuasi wake kutaka kugharamia fomu yake ya kugombea nafasi hiyo, lakini amechagua ilipiwe na mwanachama aitwaye Edgar Mwakalebela (Sativa).
“Hizi fomu zinatakiwa zilipiwe ada yake ya Sh.1,500,000 ningeilipia mimi mwenyewe, lakini kuna wanachama wema wanaofikiri kama mimi, wanaofikiri kwamba uchaguzi huu uwe mwanzo mpya kwa ajili ya chama chetu, ambao wamechanga fedha kwa ajili ya kulipita gharama hii.
Imeandaliwa na Elizabeth Zaya na Romana Mallya
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED