Aliyeng'atwa Na Nyoka... Afia kituo cha afya kisa hana 150,000/-

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 10:47 AM Dec 18 2024
Aliyeng'atwa Na Nyoka...  Afia kituo cha afya kisa hana 150,000/-
Picha: Mtandao
Aliyeng'atwa Na Nyoka... Afia kituo cha afya kisa hana 150,000/-

KATIKA hali ya kusikitisha, mkazi wa Magugu, Wilaya ya Babati, Juliana Obedy (44), amepoteza maisha baada ya wataalamu katika Kituo cha Afya Magugu, kudaiwa kumcheleweshea huduma kituoni hapo kutokana na kugongwa na nyoka.

Imedaiwa kuwa, sababu za kucheleweshwa kwa huduma hiyo ni wataalamu kutaka kulipwa Sh. 150,000 ikiwa ni gharama za matibabu.

Akisimulia mkasa huo jana, mume wa Juliana, Obedy Laizer, alisema Desemba 16, mwaka huu, akiwa anavunja jengo la Kanisa la Katoliki Magugu, mke wake alipita akiwa anachuma mboga za majani na kung'atwa na nyoka ambaye hakujua ni wa aina gani.

Laizer alisema baada ya muda mfupi mke wake kuondoka, alikuja mtoto wake na kumwambia anaitwa na mama yake ambaye alidai kung'atwa na nyoka, ndipo alipokimbia kumpeleka Kituo cha Afya Magugu.

Alipomfikisha kituoni hapo kulikuwa na foleni na kushauriana na mke wake waingie ndani na kujisajili, lakini wauguzi waliwaambia kuwa daktari alikuwa chumba cha wazazi na kuomba apigiwe simu ili kuja kumsaidia.

"Daktari alipigiwa simu mara ya kwanza hakupokea, akapigiwa simu mara ya pili ndipo alipopokea akasema anakuja na alitoa huduma na mgonjwa kuandikiwa dawa," alisema Laizer.

Hata hivyo, alisema alipoenda duka la dawa aliambiwa anatakiwa kulipia Sh. 150,000 ambapo Laizer aliomba mgonjwa ahudumiwe na fedha itafuata, lakini wauguzi wawili na daktari mmoja waliokuwapo hawakukubali na kuamua kumpigia Mganga Mfawidhi simu na kujibiwa kuwa anatakiwa alipie Sh. 150,000 na kukata simu.

Laizer alisema baada ya kuvutana na wataalamu hao alitoka na kwenda kutafuta fedha aliporudi alitoa Sh. 130,000 na badala ya kuanza kutoa huduma, wataalamu hao walianza kupigiana simu ndipo mmoja alisikika akisema mgonjwa ahudumiwe.

Aidha, alisema baada ya kulipia fedha hiyo muuguzi anayehusika na dawa alimpeleka duka la dawa na kumpatia na walirudi kwa mgonjwa ambako alifukuzwa wodini, lakini aligoma akitaka kushuhudia mke wake akihudumiwa.

Alisema mgonjwa aliulizwa anajisikiaje naye akajibu kuwa anajisikia vibaya huku akisema “Bwana Yesu nisaidie” ghafla aliacha kuongea na ndugu na majirani waliokuwapo walianza kumwombea kwa kushirikiana naye bila mafanikio.

Alisema baada ya mke wake kukata kauli wauguzi waliendelea kumchua na kumwekea oksijen, lakini alipoona haisaidii aliwaambia waitoe.

"Baada ya kuona hivyo niliwaambia mke wangu ndio anaondoka hivyo, tulienda duka la dawa wakanipa dawa ya Sh. 6000 ya kumpunguzia maumivu na sikupewa risiti, wala ile ya 150,000 sikupewa," alisema.

Akiongea kwa uchungu alisema licha ya kuwaomba aweke rehani pikipiki yake na kuwapa funguo wauguzi ili wamhudumie mke wake waligoma na kudai akikimbia wao ndio wanawajibika.

Mtoto wa marehemu, Abednego Obedy, alisema mama yake alimwonesha mkono ukiwa umevimba na kumwambia ameng'atwa na nyoka na kumshauri kwenda kituo cha afya.

Aidha, Enoti Philipo ambaye alikuwa akimwita marehemu shangazi, alisema alitoka nyumbani kwake kuchuma mboga za majani na baadaye aliona mume wake anamkimbiza hospitali.

Mkazi wa kijiji hicho, Yona Laizer, alisema kitendo kilichofanywa na wataalamu hao ni uzembe na unyama ambao kama wakiendelea watasababisha vifo vingi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Lohay Amos, alilaani tukio hilo na kuwataka wauguzi na madaktari kutii viapo vyao.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Magugu, Dk. Kusta Ndunguru, alikiri kupigiwa simu na Laizer huku akisema alijua anathibitisha malipo aliyoambiwa.

Dk. Ndunguru alisema alimwambia aongee na wataalamu waliopo hospitali ili wamsaidie kwa kuwa yeye yuko nje ya kituo na hakumrudia.

Alisema mtu aking'atwa na nyoka mwenye sumu kali haitakiwi kuzidi nusu saa kwasababu ikizidi anapoteza maisha ndio maana alimwambia awaeleze wataalamu ili wamsaidie asipoteze muda.