WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amezindua mifumo ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mpango wa Toto Afya Kadi ambao unaruhusu mtoto mmoja kujiunga kwa hiari kuanzia Sh. 150,000.
Katika mpango huo, NHIF umefanya mapitio ya fao hilo ili liwe endelevu na stahimilivu na kwa watoto watakaoandikishwa kupitia makundi yao ya shule watachangia Sh. 50,400 kwa mwaka.
Watoto watakaojiunga kwa utaratibu wa hiyari katika chaguo la kwanza litakuwa Sh. 658,000, la pili ni Sh. 237,000 na la tatu watalipa Sh. 150,000.
Waziri Jenista alisema jijini hapa jana kuwa mpango huo awali pamoja na uzuri wake wa kusaidia wananchi ulisababisha hasara kwa kuwa kwenye kila Sh. 100 mtoto alitumia takribani Sh. 600.
"Niwapongeze kwa kuwa wasikivu na kufanyia kazi maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine kuhusu mpango wa usajili wa mtoto mmoja mmoja iwapo itatokea kwamba mtoto hayuko shuleni," alisema.
Hivyo, alitoa wito kwa wananchi kuwasajili watoto wao ili kuhudumiwa kwa utaratibu wa bima ya afya na kuhakikisha wanakuwa walinzi wa huduma ili mfuko usiibiwe kupitia huduma za watoto.
Kuhusu mifumo, alisema kuzinduliwa kwa mifumo hiyo ni mwarobaini wa vitendo vya udanganyifu vilivyokabili mfuko kwa muda mrefu.
Aliagiza maboresho ya mifumo yafanyike mara kwa mara kwa kuzingatia mazingira halisi na isizalishe tena changamoto ambazo zitaathiri uhai na uendelevu wa mfuko.
Kadhalika, aliagiza mfumo katika mchakato wa vifurushi mbalimbali vya kuwezesha wananchi kujiunga kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wahakikishe havina malalamiko ili kusaidia sekta ya afya kusimama vizuri.
Jenista alikemea tabia ya baadhi ya watoa huduma kutumia mfuko kujipatia mapato yasiyo halali kwa njia ya udanganyifu na kutaka mifumo hiyo ilindwe ili isiingiliwe na watu wajanja, isomane na taasisi nyingine na ipatikane hadi vijijini ili wananchi wapate huduma kwa urahisi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Irene Isaka alisema kwa watoto watakaojiunga kwa Sh. 150,000 kiwango cha ukomo watatumia Sh. 2,000,000 kwa wanaolazwa huku wagonjwa wa nje ni Sh. 1,000,000.
Alisema kwa watoto watakaojiunga kwa Sh. 237,000, wanaolazwa kiwango cha ukomo ni Sh. milioni nane na wagonjwa wa nje ni Sh. milioni mbili, huku kwa watakaolipa Sh. 658,000 kiwango cha ukomo ni Sh. milioni 22 na wagonjwa wa nje ni Sh. milioni tatu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu alisema NHIF ni roho ya taifa kwa sababu ustahimilivu wake unaweza kusababisha amani na utulivu wa nchi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED