Mwekezaji mzawa wa mkoani Manyara, David Mulokozi, amewashangaza wananchi wa Babati baada ya kutua na helikopta yake binafsi ambayo amenunua ili kurahisisha usafiri katika shughuli zake.
Mulokozi ameiomba serikali kujenga uwanja wa ndege mkoani Manyara au kumruhusu ajenge yeye mwenyewe, kisha serikali imlipe baadaye, ili kurahisisha usafiri wa anga. Mulokozi ametua leo Desemba 18 katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa akiwa na familia yake, akitokea ughaibuni.
Amesema gharama inayotumiwa na wananchi wa Manyara kwenda Viwanja vya Ndege vya Kilimanjaro (KIA) na Dodoma ni kubwa. Ameeleza kuwa fedha zinazotumika kusafiri kwa magari kufuata viwanja hivyo zinaweza kulipia usafiri wa ndege moja kwa moja kwenda Dar es Salaam.
Tajiri huyo ameongeza kuwa hakupata usumbufu wakati wa kufuatilia vibali vya kununua helikopta hiyo, kwani alifuata taratibu zote zinazotakiwa. “Naomba serikali itujengee uwanja wa ndege Manyara ili kurahisisha usafiri. Kama itaniruhusu kujenga mwenyewe, niko tayari kuanza hata kesho, maana huu ni uwekezaji,” amesema Mulokozi.
Mulokozi ameweka wazi kuwa helikopta hiyo itarahisisha biashara zake, hususan za kiwanda chake cha Mati Super Brands Limited, kwani sasa ataweza kusafiri mikoa saba hadi 10 kuonana na wateja wao kwa urahisi. Ameeleza kuwa ameonyesha njia kwa wafanyabiashara wengine wa Manyara wenye uwezo wa kununua ndege binafsi, ili kuongeza wigo wa usafiri wa anga mkoani humo.
Baada ya kutoka Babati, ndege hiyo itaelekea Bukoba mkoani Kagera, ikipitia Mwanza kwa ajili ya kuongeza mafuta, kisha kurejea Babati kabla ya kupaki Arusha au KIA.
Mkazi wa Babati, Inyasi Melicholi, alimpongeza Mulokozi kwa hatua hiyo ya uthubutu, akisema kuwa ameiheshimisha Babati na Mkoa wa Manyara kwa ujumla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED