Mamia ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na nje ya mkoa huo wamekusanyika nyumbani kwa mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe, kumuomba achukue fomu ya kutetea nafasi yake hiyo kwa mara nyingine.
Gazeti la Nipashe limeshuhudia magari ya kukodi maarufu kama 'Special Hire' yakishusha wafuasi wa chama hicho, ambao wengi walikuwa wamevalia sare za chama na kubeba bendera zake.
Tayari chama hicho kimeanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya taifa na mabaraza yake, ikiwemo nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar, pamoja na nyinginezo. Hadi sasa, Mbowe hajatangaza kama atagombea tena nafasi hiyo au la.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti Bara wa sasa wa chama hicho, Tundu Lissu, tayari ametangaza nia yake na ameshachukua fomu ya kugombea. Jana, baada ya chama kutangaza kuanza kwa mchakato wa uchaguzi, Lissu alichukua fomu ofisini Mikocheni, Dar es Salaam, na leo anatarajiwa kuirejesha.
Uchaguzi huo wa CHADEMA umepangwa kufanyika Januari mwaka kesho.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED