WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imetenga Sh.bilioni 216 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Utoaji wa Chanjo na utambuzi wa Mifugo Kitaifa utakaoanza Januari 2025 utakaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2024-2029 ambapo Sh. bilioni 28.1 zitatumika awamu ya kwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk.Ashantu Kijaji, akizungumza leo Desemba 18, 2024 kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa amesema mpango huo unalenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeridhia kugharamia mpango wa chanjo wa miaka mitano kuanzia 2024 hadi 2029 ambapo mifugo itachanjwa kudhibiti ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng'ombe, ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na ugonjwa wa mdondo wa kuku ili kuwasaidia wafugaji wetu kote nchini," amesema.
Dk. Kijaji amesema awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo Serikali kupitia wataalamu wa Sekta ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa itachanja ng’ombe 19,097,223 dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe (CBPP), Mbuzi na Kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) na kuku wa asili 40,000,000 watachanjwa dhidi ya ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED