UJENZI wa jengo la kutoa huduma ya mama na mtoto uliofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kituo cha Afya cha Makole, Jijini Dodoma, umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa eneo hilo, kwani sasa wanapata huduma katika mazingira bora na rahisi.
Kabla ya ujenzi wa jengo hilo, wananchi wa Kata ya Makole na maeneo ya jirani ya Swaswa na Ipagala walikuwa wakipata huduma za mama na mtoto, ikiwa ni pamoja na chanjo, kwenye turubai lililokuwa limefungwa katika kituo hicho. Hali hii ilichangia mazingira yasiyofaa na huduma kutolewa bila ya usalama na ufanisi.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa Kata ya Makole, Suzan Yohana, amesema kuwa kabla ya jengo kujengwa, wananchi walikuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo mvua za msimu na vumbi wakati wa kiangazi, pamoja na kukosa hewa safi kutokana na ufinyu wa eneo. Aliendelea kusema, “Kata ya Makole ni kubwa sana, hivyo watu walikuwa wanatoka maeneo mbalimbali kuja kupata huduma. Hali ya mazingira ya utoaji huduma haikuwa rafiki kwa sababu turubai lilikuwa halifai kwa matumizi. Lakini sasa, tunashukuru tumepata jengo zuri na wananchi wanapata huduma katika mazingira mazuri.”
Suzan aliongeza kuwa TASAF imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuboresha huduma za mama na mtoto, na kwamba sasa huduma zinatolewa kwa wepesi katika mazingira safi na salama.
Joyce Kimario, Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Makole, alisema kuwa kabla ya jengo hili, idadi ya wananchi waliokuwa wakija kupata huduma ilikuwa ndogo, lakini kwa sasa idadi imeongezeka kwa kiasi kikubwa. “Siku za nyuma, huduma za chanjo ya mama na mtoto chini ya miaka mitano zilikuwa zinatolewa kwenye turubai, lakini baada ya TASAF kujenga jengo hili, idadi ya wanaokuja kupata huduma imeongezeka. Tunawashukuru TASAF kwa msaada wao na tunaomba waendelee kuboresha majengo ya idara nyingine,” alisema Joyce.
Muuguzi Mkunga katika kituo hicho, Tumain Myeule, alisema kuwa wananchi wanashukuru kwa kuboreshwa kwa huduma, na kwamba mazingira ya utoaji huduma sasa ni bora zaidi. Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuendelea kufaidika na huduma hizo.
Mwanakamati anayeshughulikia mpango wa walengwa wa TASAF ngazi ya mtaa, Neema Tandi, alisema kuwa wananchi wa Kata ya Makole, ambao ni walengwa wa jengo hilo, wanapata huduma za mama na mtoto bila ya usumbufu. “Wakati wa turubai, kuna muda huduma zilikuwa zinasimama kutokana na upepo au mvua, lakini sasa tuna jengo hili ambalo linatoa huduma za chanjo kwa ufanisi,” alisema Neema.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Makole walitoa pongezi kwa TASAF kwa kuona umuhimu wa kujenga jengo hili, ambalo limewezesha huduma kutolewa katika mazingira bora. Eliza Mazengo, mama wa mtoto wa miezi mitano na mkazi wa Makole, alisema, “Tunashukuru sana kwa jengo hili. Sasa tunapata huduma ya mama na mtoto kirahisi. Tunaomba tu TASAF iendelee kuboresha majengo ya wajawazito, kwa sababu kituo kinahudumia watu wengi.”
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED