Kikwete: Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa vijana

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:57 PM Dec 18 2024
Kikwete: Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa vijana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kikwete: Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa vijana.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa vijana ikiwemo kuwekeza katika maeneo mengi kama elimu, afya, na mambo yote ya ustawi wa jamii ili kuhakikisha wananufaika.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam, wakati wa mkutano na mtandao wa vijana uliolenga kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ridhiwani amesema kuna haja ya vijana kujitokeza kutoa maoni ya dira hiyo ili kuboresha zaidi sekta hizo kulingana na matakwa yao.

"Nini maoni yenu vijana juu ya haya yanayofanyika leo kwa ajili ya kesho yetu, hili ndilo jambo tunalolitaka kulisikia kutoka kwenu vijana ili tuweze kuona kipi cha kufanya," amesema Ridhiwani.

Amesema katika maoni mbalimbali yaliyotolewa na vijana, wengi wamezungumzia kwa ukubwa uhitaji wa kuimarisha afya ili nguvu kazi ya vijana ipate kuimarishwa na kuwa na tija kwao na kwa taifa kwa ujumla kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

"Maeneo ambayo yamefanyiwa kazi katika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Mwaka 2007 ambayo yamefanyiwa marejeo mwaka 2024, ni pamoja na elimu na ujuzi, uvumbuzi na ubunifu, na mapinduzi ya kidijiti. Mambo haya yanaweza kuchambuliwa katika kipindi kama hiki cha kutoa maoni ya dira," amesema Ridhiwani.

1