SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inatarajia kugawa vyandarua 841,503 bure kwa wananchi wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa wa malaria na kuwasisitiza wale watakaovipata wahakikishe wanavitumia katika matunzi yaliyopangwa nasio kufugia kuku.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita aliyabainisha hayo wakati wa kikao cha maandalizi ya kampeni ya ugawaji wa vyandarua kwa ngazi ya kaya, inayotarajia kuanza Januari 16 mwakani na vitatolewa kupitia ofisi za watendaji wa kata pamoja na vijiji na kila kaya itapata kulingana na idadi yake.
Amesema, jumla ya vyandarua 841,503 vitatolewa Wilaya ya Kahama pasi kuwa na malipo ya aina yoyote ambapo Halmashauri ya Msalala itapata vyandarua 260,350, Ushetu 268,872 na Manispaa ya Kahama 312,836 lengo likiwa ni kukabiliana na ugonjwa wa malaria.
Hata hivyo aliwaonywa watendaji hao kutokuuza vyandaru vitakavyotolewa nabadala yake wavigawe bila ubaguzi ili viwafikie wote na kutimiza lengo la kukabiliana na ugonjwa huo kwenye jamii.
Ofisa mradi mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria, Wilfred Mwafungo amesema,kwa mujibu za kitaifa za viasharia vya malaria mwaka 2022 kiwango cha kitaifa cha maambukizi ni asilimia 8.1 ambapo mkoa wa Tabora unaongoza ukiwa na asilimia 23.4 ukifuatiwa na Mara asilimia 20 na shinyanga kwa asilimia 16 na ndio sababu ya serikali kutoa vyandarua bure kwa kila kaya ili kupambana na ugonjwa huo.
Mthibiti wa wadudu dhurufu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI,Best Yoram amewataka wananchi kuacha kutumia dawa pasi kupima na kujua anaumwa nini kwani baadhi yao wamekuwa wakiumwa kichwa na kuhusisha na moja ya dalili ya ugonjwa wa malaria na kuanza dozi pasi kupima jambo ambalo ni hatari kiafya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED