Watu 14 wafariki, nane wajeruhiwa ajalini Mikese

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 11:45 AM Dec 18 2024
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima.

WATU 14 wamefariki dunia na wengine nane kujeruhiwa baada ya magari waliokuwa wakisafiria, basi dogo aina ya Costa na lori la mizigo, kugongana uso kwa uso usiku wa kuamkia leo katika eneo la Mikese wilayani Morogoro, barabara kuu ya Morogoro - Dar es Salaam.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Daniel Mkungu, amesema walipokea majeruhi nane na miili ya watu 14 waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alifika hospitalini hapo usiku huo kuwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo. Malima alisema kuwa ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa madereva, ambao wote wawili wanadaiwa kupoteza maisha katika ajali hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa aliwasihi madereva kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima zinazogharimu maisha ya watu na mali zao. Pia aliwataka wananchi kufika hospitalini hapo kutambua miili ya marehemu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Jitihada zaidi zinaendelea kufanywa kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, ili azungumzie kwa kina kuhusu ajali hiyo.