Neema ya ajira 45,080 kutolewa 2024/25

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:21 PM Dec 18 2024
Ajira.
Picha: Mtandao
Ajira.

SERIKALI imesema katika Mwaka 2024/25 imetoa kibali cha kuajiri watumishi 45,080 wa kada mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alipokuwa akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Rasilimaliwatu na Utawala katika utumishi wa umma kutoka kwenye Wizara, Wakala, Mamlaka, Mashirika na Taasisi za serikali Serikali.

Amesema kwa kutambua kuwa Rasilimaliwatu ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa, serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira kwa kada mbalimbali na kwa Mwaka huu kati ya idadi hiyo ya watumishi 10,396 ni wa kada za Afya na 10,590 wa kada za ualimu huku 24,094 ni wa kada nyingine.

“Aidha, nimetaarifa kuwa mchakato wa ajira wa watumishi wa kada za afya umekamilishwa na watumishi hao tayari wameshapangiwa vituo vya kazi. Niwatake waajiri kuhakikisha wanawapatia mafunzo ya awali, kuwalipa stahiki zao na wanawajengea uwezo,”amesema

Vilevile, amesema ni wajibu wa waajiri wote kutenga bajeti kwa ajili ya ajira mpya kulingana na mahitaji halisi ya taasisi zao.