Makamu Rais Z'bar: Utitiri wa kodi na wasimamizi wengi vinawatesa walipaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:08 PM Dec 18 2024
Makamu Rais Z'bar: Utitiri wa kodi na wasimamizi wengi vinawatesa walipaji.
Picha:Mtandao
Makamu Rais Z'bar: Utitiri wa kodi na wasimamizi wengi vinawatesa walipaji.

TUME ya Rais ya Maboresho ya Kodi imekutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, ili kujitambulisha.

Tume hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Balozi Ombeni Sefue na ujumbe wake, walijadili mambo mbalimbali ikiwamo mapendekezo yatakayozishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kuhusu masuala ya kodi.

Akizungumza baada ya kuupokea ujumbe huo, Dk. Mwinyi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiteua tume hiyo ambayo alisema itasaidia kuimarisha na kubadilisha mifumo ya kodi kwa serikali hizo na kuleta mageuzi kwenye biashara hususani eneo la kodi.

Wakati huo huo, Tume hiyo ilikutana na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman.

Othman, alitahadharisha kuwa mfumo wa kodi uliopo nchini unaruhusu utitiri wa kodi nyingi kusimamiwa na mamlaka tofauti na kuhatarisha kuanguka kwa biashara nchini.

Alisema kuwapo kwa mamlaka nyingi za kodi mbali na kusababisa usumbufu kwa wafanyabiashara nchini ni changamoto kubwa ambayo ni muhimu kwa tume hiyo kuangalia upya, hususani katika sekta ya uchumi ikiwamo usafiri wa anga na huduma katika sekta ya kilimo.

Alisema kuna haja kwa Tanzania kubadili mwelekeo wa mfumo wa kodi ndani ya nchi ili kurahisisha shughuli za kodi na biashara ili kwenda kwa wepesi zaidi kuliko ilivyo sasa.

Aidha, licha ya taifa kujitahidi kukuza sekta mbalimbali ni vyema kuangalia mfumo sahihi wa kodi katika kilimo jambo litakalochangia rasilimali zilizomo kuwekezwa na kuleta tija ndani ya Tanzania.

Alisema hali ilivyo sasa inaweza kuchangia baadhi ya wafanyabiashara kushindwa sio tu kulipa kodi kikamilifu na nchi ikapata tija, lakini kutoendelea na shughuli za kibiashara jambo linalohitaji kuangaliwa kwa makini.

Akizungumzia suala la kodi katika sekta ya usafirishaji wa anga, Othman alisema Tanzania imeshawahi kuwa na kampuni nyingi ambazo zinatoa fursa nyingi za ajira, lakini bado ni eneo linalohitaji kurekebishwa zaidi katika mfumo wa kodi ili kusaidia tija zaidi kwa manufaa ya nchi. 

Alisema kutokana na hali hiyo hivi sasa, usafiri wa anga umekuwa ni biashara na huduma inayoweza kutumiwa na watu matajiri pekee jambo ambalo linahitaji kuangaliwa zaidi ili sekta hiyo ya anga iweze kukua zaidi.

Kadhalika, alishauri kwamba kutokana na mazingira ya Tanzania kunahitajika kuwapo mfumo wa kodi unaolenga hali halisi ya nchi ili kusaidia nchi katika kukusanya kodi na kuchangia ukuaji wa uchumi kama zinavyofanya nchi nyingine.

Pia, alishauri kuwapo na mamlaka chache za kodi ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara kusimamiwa na taasisi nyingi za kodi jambo litakalochangia kukua kwa biashara ndani ya nchini.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue, alisema kwamba imepewa jukumu la kukutana na wadau ili kuangalia mfumo wote wa kodi na kuwasilisha serikalini mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kodi Tanzania.

Alisema kwamba hatua hiyo ni kuisaidia serikali kufanya marekebisho na kuufanya mfumo wa kodi ulipo nchini kuwa rahisi na kuweka mazingira mazuri ya kibiashara Tanzania.