Waziri Ulega: TANROADS msilale

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:16 PM Dec 19 2024
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega.

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewasisitiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi ya dharura iliyo chini yake.



 
Akizungumza wakati wa mkutano wake na menejimenti na mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini uliofanyika leo mkoani Dodoma, kiongozi huyo alisisitiza kwamba ni muhimu miradi ya dharura ikawekewa kipaumbele cha kushughulikiwa kidharura. 
 
“Fanyeni kazi kwa kasi tena usiku na mchana hususani kwenye miradi ya dharura ili kuwawezesha Watanzania kuondokana na adha ya miundombinu iliyoharibiwa,” amesema Ulega.
 
Pia amesisitiza menejnmenti hiyo kwamba wanatakiwa waende kwa spidi inayofanana na viwango vya kasi vinavyoonekana wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linapopewa majukumu ya utekelezaji na serikali kwa sababu kuna mvua zinakuja na zinaweza kufanya maeneo yaliyoharibika kuharibika zaidi.
 
Amesema barabara zilizoharibika kwa sababu ya mvua za masika zilizochanganyika na zile za El Niño zimesababisha usumbufu na kusimamisha shughuli za uchumi na hivyo ni muhimu zikashughulikiwa kwa haraka.
 
Aidha, Waziri Ulega amewapongeza wafanyakazi wa TANROADS kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi ambako katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imekamilisha ujenzi wa barabara kwa zaidi ya kilometa 1,198 kwa kiwango cha lami.