Vijana wataka umri wa kustaafu uwe miaka 50

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:19 PM Dec 19 2024
Omary Punzi ambaye ni Mratibu wa Makongamano ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 Toleo la Mwaka 2024

BAADHI ya vijana waliotoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, wameshauri serikali kushusha umri wa kustaafu hadi miaka 50 kwa hiari na 55 kwa lazima kutoka 60 inayotumika sasa, ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuingia katika mfumo wa ajira.

Akitoa maoni yake jana mkoani Dar es Salaam, Omary Punzi ambaye ni Mratibu wa Makongamano ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 Toleo la Mwaka 2024, alisema serikali inapaswa kuliangalia hilo kwa ukaribu ili vijana nao wale keki ya taifa.

Alisema ni vyema sekta binafsi nayo itengeneze mfumo wa maombi ya ajira kama ilivyo kwa mfumo wa Ajira Portal wa serikali, ili kijana anapotaka kwenda kujiunga na sekta hiyo aone ushindani, akidai kuwa sekta za umma kukitokea fursa zinatangazwa, lakini binafsi hali ni tofauti. Chache hutangazwa.

"Kadhalika, tunaona sasa hivi umri wa kuingia jeshini ni miaka 25, lakini tuna mfumo ambao serikali ilianzisha wa elimu ya watu wazima, lakini mfumo wa kuingia jeshini haujawapa kipaumbele wale ambao wanamaliza katika umri wa watu wazima.

"Ni vyema umri wa kuingia jeshini ukasogezwa ukafika angalau kuanzia miaka 30 ili wale ambao wamemaliza elimu ya juu wakiwa ndani ya umri huo wapate muda wa kujiunga na kulitumikia taifa lao," alishauri Punzi, ambaye pia ni Mratibu wa Shughuli za Skauti Mkoa wa Pwani - Idara ya Kazi Maalumu.

Naye Saimon Chambi alishauri kwamba kuelekea mwaka 2050, kuwapo jukwaa na mkakati maalumu wa kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za ajira na programu za kimataifa za kubadilishana uzoefu kama sehemu ya kuondoa kundi hilo katika changamoto ya ajira.

Alisema asilimia tano pekee ya vijana ndiyo wanaonufaika na fursa mbalimbali za mafunzo na ajira nje ya nchi na hivyo kutaka kuundwa kwa mkakati maalumu kuwawezesha kupata taarifa sahihi za fursa hizo na kutengenezwa njia nyepesi kwa kundi hilo kujiunganisha na ajira na mafunzo.

"Dira ya 2050 iainishe namna ambavyo vijana wanaweza kupata mafunzo mbalimbali ya mambo yasiyofundishwa kwenye taasisi rasmi za elimu, ikiwamo afya ya uzazi, elimu ya fedha na mengineyo ili kusaidia kundi hilo kujitambua na kutumia vyema rasilimali fedha kidogo wanazopata kwa njia mbalimbali," alishauri Chambi.

Gipson Kawago, akitoa maoni yake, alishauri kuwe na mkazo katika elimu ya vitendo zaidi kuliko nadharia, akisisitiza kuwa hiyo itawasaidia vijana baada ya kuhitimu kuwa rahisi kujiajiri.

"Kuna uhaba wa miundombinu rafiki ya kumwaandaa kijana kuwa na utaalamu wa kivitendo. Pia kuwe na utaratibu wa kuwafundisha wanafunzi kuhusu akili mnemba kuanzia shule za msingi ili isiwe jambo geni kwao wanapofika ngazi za juu, kwa sababu teknolojia inaendelea kukua," alisema Kawago.

Joseph Malekela alisema dira haijaonesha namna gani nchi imeweka mikakati ya kuwaandaa vijana katika kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya uongozi, akishauri ni muhimu dira kuonesha utaratibu rasmi kufikia mwaka 2050 vijana watashiriki kwa kiasi gani katika nafasi za uamuzi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema atahakikisha kundi la vijana linaendelea kuwa sehemu ya wanufaika wa keki ya taifa kwa kufanyia kazi mawazo yao.

"Niwahakikishie kwamba mimi kama waziri wa vijana, nitayasimamia yale ambayo mmeyasema na nitahakikisha yote yaliyosema yanaakisi katika huo mpango mkubwa unaotakiwa kwenda kutokea. Moja ya vipaumbele vya Rais Samia Suluhu Hassan kuniteua ni ili kwenda kushughulikia changamoto za vijana," aliahidi.