MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema atatoa msimamo wake ndani ya saa 48 zijazo kama atagombea tena nafasi hiyo au la.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya kuombwa na makada, wanaojumuisha wenyeviti wa chama hicho katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na wafuasi wengine waliofurika nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam.
"Nimesikia na ninaheshimu maombi yenu. Nimepokea maombi na ushauri kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanachama na wasio wanachama wakiwamo viongozi wa dini.
"Ninawaomba mnipe muda, nitaangalia ndani ya saa 48 nitatoa msimamo wangu mbele ya wahariri wa vyombo vya habari. Kama nitaona mambo hayaendi vizuri, mwamba nitaingia tena mzigoni," alisema Mbowe.
Kuhusu msuguano wa makundi ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi, Mbowe alisema hafurahishwi na hali hiyo na anawataka wanachama kuacha mivutano hiyo bali wawe kitu kimoja na waangalie mbele katika kujenga taasisi hiyo.
"Sijapenda makundi namna yanavyoendelea kusigana, kununiana, kuchukiana na pengine kusema uongo. Chama hiki kinaongozwa na vikao na si matamko ya Mwenyekiti Mbowe, mimi ni kiongozi tu.
"Anapotoka kiongozi aliyekaa miaka 20 madarakani na kusema jambo la tofauti, tunaanza kufikiri labda mwenzetu hatukuwa pamoja, kila mtu anayetafuta uongozi atafute lakini katika mazingira ya kuwajenga wenzake na kuilinda hii taasisi," alitoa angalizo.
Mbowe alisema amekuwa na wakati mgumu na familia yake inamshawishi kuachana na siasa, huku wanachama wa CHADEMA wakimshawishi kuendelea kuongoza chama hicho.
UCHAGUZI
Akizungumzia uchaguzi ndani ya chama hicho, Mbowe alionya makundi kusigana na kuchafuana kwa kutumia uongo, huku akitamba historia ya uongozi wake ndani ya chama inambeba.
Hivyo, aliwataka wanachama wa chama hicho kulinda chama hicho kwa wivu mkubwa, kutokuwa na kinyongo na mtu yeyote pasipo kufanya ulipizaji kisasi na kwamba hata yeye amewasamehe wote waliokuwa wamemtukana na kumdhalilisha kwa maneno mbalimbali katika mitandao ya kijamii.
Mbowe alisema: "Kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tusiwadhalilishe wenzetu kwa kuwa ni askari wenzetu na wapiganaji wenzetu. Mimi nimewasamehe wale wote waliokuwa wananitukana na wanaoendelea kunitukana."
ILIVYOKUWA NYUMBANI
Nje ya nyumba ya Mbowe, baadhi ya wafuasi wa chama hicho pamoja na wenyeviti kutoka katika zaidi ya mikoa ya kichama 20, ni miongoni mwa waliojitokeza kumwomba na kumshawishi mwanasiasa achukue fomu ya kutetea tena nafasi yake.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Iringa, William Mungai alisema watamuunga mkono Mbowe katika uchaguzi wa kitaifa wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Januari mwakani ikiwa atagombea.
Viongozi hao pamoja na mamia ya wafuasi walifika nyumbani kwa Mbowe saa nne asubuhi, baadhi wakitumia magari binafsi, mabasi madogo ya abiria (coaster) na bodaboda. Walifurika nyumbani kwake.
Saa 9:25 alasiri Mbowe alitoka ndani ya nyumba yake kuwasikiliza wafuasi hao pamoja na wenyeviti. Hapo ndipo Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Mungai, aliposema kuwa kutokana na ubunifu wa Mbowe, CHADEMA imeendelea kuwa imara kwa miaka mingi.
Mungai alitaja sababu zilizowasukuma kumwomba mkongwe huyo wa siasa agombee tena nafasi yake, ni ububifu wa operesheni mbalimbali ambazo zimewezesha chama hicho kupata wanachama, zikiwamo Operesheni Sangara na Movement for Change na kwamba hawana uhakika na wagombea wengine iwapo watasaidia katika kuongeza wanachama.
Alisema amebuni nguo, bendera na alama nyingine za chama ambazo zimepata umaarufu na zinatumika mpaka leo.
Mungai alisema Mbowe ana uwezo wa kujenga viongozi ambao wengine wamechukuliwa na vyama vingine na kuwa viongozi katika vyama hivyo, wengine kupata uongozi serikalini; wakijumuisha wakuu wa wilaya, mikoa na hata mawaziri.
Alisema Mbowe ni 'States Man' na jasiri wa vita asiyeogopa mapambano na siyo mtu wa matamko tu kama wengine, akitolea mfano alivyoweza kujitokeza katika maandamano waliyoyatangaza miezi iliyopita, tena akiwa na binti yake.
Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Ally Kadogoo alisifu uongozi wa Mbowe kuwa ni wa kutoa fursa sawa kwa watu wote, akijitolea mfano, kwamba alipotoka, hakuwahi kuwa hata mjumbe wa mtaa lakini hivi sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani.
LISSU ARUDISHA FOMU
Wakati wafuasi wakijitokeza nyumbani kwa Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu jana alirudisha fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Lissu alifika katika makao makuu ya chama hicho majira ya mchana na kupokewa na Naibu Katibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Benson Kigaila.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED