Yabainika malezi ya akinamama chanzo ukatili

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 02:10 PM Dec 19 2024
Waadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani
Picha: Yasmine Protace
Waadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani

IMEELEZWA kuwa asilimia 90 ya akinamama wana kasoro kwenye malezi na hivyo kuchangia watoto wao kufanyiwa matukio ya ukatili.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Jumuiya wa Wanawake Mkoa wa Pwani, Mushanga Said katika maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Kibaha Vijijini, yalifungwa na katibu huyo, akisema matukio ya ukatili yamekuwa yakitokea kwa watoto kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa malezi.

"Asilimia 90 ya akinamama wanachangia mapungufu katika malezi ya watoto wao, baadhi ya akinamama wanatumia muda mwingi kutafuta kipato badala ya kusimamia malezi.

“Akinamama wanapopata shida ya kipato huwatuma watoto wa kike kufanya biashara katika biashara watoto hubakwa.”

Kamishna wa SMAUJATA Taifa, Amos Nzoa,  aliishukuru CSSC kwa kuwawezesha mchango wao, ili kufanikisha kusherehekea maadhimisho hayo.

Alisema SMAUJATA ilianza mwaka 2022 na wamekuwa wakihakikisha taasisi yao inafika mbali katika kupambana na matukio ya ukatili hapa nchini.

“Taasisi ya  CSSC imekuwa na mchango mkubwa katika ulinzi na usalama wa mtoto kupitia mradi wa UWAWA. Kupitia mradi huo imekuwa ikijengea uwezo shule ,walimu na walezi pamoja na wanafunzi katika kutambua haki za watoto na masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto.”

Waadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kibaha, Yahaya Mbongole, alisema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024 , matukio 1,010 ya ukatili yameripotiwa.

Alisema matukio ya kihisia 483 na ya kimwili 337 huku 111 yakiwa matukio ya ukatili wa kingono, na miongoni mwake watu 44 walifika ndani ya saa 74 kwenye vituo vya kutolea huduma huduma za afya.

"Wateja 665 walipatiwa ushauri nasaha, wateja 37 walipewa huduma za PEP na 148 walipewa huduma ya kipolisi pia 416 walipata rufaani kwenda katika maeneo ya huduma za kisheria.

Aliongeza kuwa halmashauri imekuwa ikifanya jitihada  kwa kuendelea na kampeni za kupambana na ukatili, ikiwamo kutoa elimu kupitia mikutano ya hadhara kwa kushirikiana na SMAUJATA.