Mwanachuo na wenziwe wanne mbaroni tuhuma ‘tuma kwa namba hii’

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 02:56 PM Dec 19 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi
Picha: Hamida Kamchalla
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi

VIJANA watano akiwamo mwanafumzi wa Chuo cha Arusha (IAA), wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, kwa tuhuma za wizi wa mtandaoni wakitumia mbinu za ulaghai kwa kutumia namba zilizosajiliwa kwa majina tofauti.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Peter Babuya (20) mkazi na mwanafumzi wa (IAA) Arusha; Said Amiri (21); Athumani Amiri (24); Brayan Mayunga (26) na Wakala wa huduma za fedha za mitandao, James Nathaniel (24).

Kamanda amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini, jijini Dar es Salaam, Mtwara na wilayani Masasi baada ya kudai kuwa ni mawakala wa kujitegemea.

"Lakini pia katika hatua nyingine tumefanikiwa kukamata wahamiaji haramu watatu kutoka nchini Ethiopia, kuanzia Novemba hadi Desemba 18, mwaka huu, katika kuimarisha misako tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 95 wakiwa na makosa mbalimbali," amesema.

"Jeshi la Polisi mkoani hapa linatoa onyo kwa wote wanaojihusisha na makosa ya jinai na kimtandao, kuwa hawatoachwa salama bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria, msako huu unaendelea, ili kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria," amesisitiza.