Vituo 47 vya kufundisha Kiswahili vyaanzishwa

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 11:59 AM Dec 19 2024
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi.
Picha: Mtandao
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Paramagamba Kabudi amesema serikali kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania, imeanzisha vituo 47 vya kufundisha lugha ya Kiswahili ili kukuza na kueneza lugha hiyo duniani.

Alisema hayo wakati akifungua kongamano la siku mbili la kimataifa la utamaduni lijulikanalo kama Afrika ya Kesho linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Jordan (JUCO) mjini Morogoro. Kati ya vituo hivyo, 17 viko nje ya Tanzania.

Alisema taasisi za elimu ya juu kupitia vijana zinaendelea kufanya utafiti na kuibua mijadala ya kutafuta urithi wa utamaduni unaoshikika na usioshikika ili kusaidia kurudisha utamaduni wa kiafrika kwa maslahi mapana ya bara la Afrika.

Msemaji Mkuu wa kongamano hilo linaloandaliwa na vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Tanzania, Prof. Anna Tibaijuka alisema kuwa na lugha moja ya asili kunabeba vitu vingi vya kiutamaduni, hivyo Afrika haipaswi kupoteza Kiswahili na kwa kufuata lugha za kigeni.

"Hatuwezi kuondoa lugha hii kwa namna yoyote ile, lazima tulinde Kiswahili, lakini na lugha zetu za makabila yote, na kwenye hili lazima tusiweke ukabila," alisema Prof. Tibaijuka.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jordan, Bertram Mapunda alisema kizazi cha sasa kinaamini kuwa mambo ya utamaduni na kuzungumza lugha za asili ni wazee wa zamani na siyo wa sasa, hivyo akawataka vijana kujifunza lugha za asili ili kusaidia kukuza na kueneza lugha hiyo.

Kuhusu elimu ya juu, Mapunda alisema wanakusudia kuanzisha mitaala watayoweza kuingiza namna ya kufundisha lugha za asili kwa wanafunzi ili kuendelea kukuza na kueneza lugha hizo.

Kiongozi wa kimila kutoka kabila la Maasai, Chifu Mtayani Simanga alisema kupitia kongomano hilo viongozi wa asili walikusudia kuonana na viongozi wa nchi ili kuwaeleza namna sahihi ya watu kuishi majumbani ili kurejesha hali ya amani na utulivu katika bara la Afrika.

Kongamano hilo limeandaliawa na Chuo Kikuu cha Jordan JUCO kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Waislamu (MUM), Chuo Kikuu cha Zanzibari, Chuo Kikuu cha Zimbabwe, Chuo Kikuu cha Nigeria na Taasisi ya Arizona ya Marekani (PPEP).