VIONGOZI mbalimbali wa dini na wadau wa siasa wametoa tathmini kuhusu kilichojiri katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Wamesema licha ya malalamiko ya raia na watu wenye nia njema, serikali haikuchukua hatua zozote za kurekebisha.
Rais wa Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa, aliyasema hayo jana katika mkutano uliokutanisha viongozi hao wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ya kikristo nchini katika ukumbi wa TEC Kurasini, Dar es Salaam.
Maaskofu hao pamoja na wadau wengine wa masuala ya amani na haki, wamekutana kufanya tathmini ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, mwaka huu, chini ya mada isemayo, ‘Je, Uamuzi wa Wapigakura Umeheshimiwa?’.
Akisoma tathmini hiyo, Pisa alisema: “Maeneo mengine tukiri uchaguzi ulifanyika kama mchezo mchafu uliosababisha vifo vitisho, rushwa, ufisadi, upendeleo, wizi wa kejeri kwa wapigakura na wagombea.
Licha ya malalamiko ya raia na watu wenye nia njema, serikali haikuchukua hatua zozote. Hii ni tabia mbaya sana inayobomoa taifa, maadili ya kisiasa, kiuchumi na kuharibu mfumo wa uwajibikaji kwa viongozi wa raia.”
Askofu Pisa alisema kupata viongozi kwa mtindo huo ni wananchi kupewa viongozi ambao hawakuwachagua.
“Imefika mahali kila inapotokea uchaguzi thamani ya utu, uhai na maisha ya Mtanzania vinashushwa kwa utekaji, mauaji na aina yote ya ukatili,” alisema.
Askofu Pisa alisema wakifungamana na ukweli na kuusimamia, utawafanya wawe huru dhidi ya mambo mbalimbali na nchi yao.
“Tufanye tafakari mbalimbali tukijua tunawajibika mbele ya Mungu, mbele ya watu na mbele ya taifa letu, Mungu ambaye hadanganyi wala hadanganyiki atuongoze,” aliwaeleza washiriki wa mkutano huo.
Askofu Pisa alisema uchaguzi wowote unaofuata mwongozo wa kikatiba na kisheria ni tendo linalohusisha uhuru, haki na dhamiri ya raia husika. Alisema ili kuhakikisha haki ya raia inaheshimika, mchakato wote wa uchaguzi husimamiwa ili ufanyike kikatiba.
“Ibara ya 3,5, 21 ili kuhakikisha hili yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa, moja, wenye sifa za kupiga kura wameandikishwa, pili, wagombea wenye sifa ya kuomba na kuteuliwa kwa mujibu wa vyama husika.
“Tatu, kampeni za wagombea na ushindaji wa vyama hufanyika kwa haki na katika fursa sawa bila upendeleo wowote, nne, wapiga kura husikiliza kampeni ili kufanya uamuzi wa msingi wa hoja na uwezo wa wagombea katika kuongoza,” alisema.
“Tano, wapiga kura huwekwa katika mazingira ya faragha ili kuheshimu usiri wa kura yao wakiamini baada ya kupiga kura inahesabiwa kwa haki na katika uangalizi wa haki uliokubalika,” aliongeza.
Alitaja jambo la sita ni wasimamizi na waratibu kuheshimu uamuzi wa kila mpigakura na saba, vyama kuwa na mawakala wao, kushuhudia upigaji kura kwa heshima, faragha na usiri bila bughudha au vishawishi vya aina yoyote.
“Nane, matokeo ya kweli ya uchaguzi huthibitishwa na vyama husika na kutangazwa bila kuingiliwa na chombo kingine na tisa, kuwa na fursa ya kuhoji na kupinga matokeo kama kuna shida au dosari”.
Askofu Pisa alisema wameshuhudia katika uchaguzi huo, hivyo ni juu yao kujiuliza yaliyotajwa ndiyo yaliyofanyika.
“Tuliyasikia matokeo ya uchaguzi yaliyotolewa na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria zetu. kila mmoja anaweza kujibu swali hili, Je, uchaguzi na matokeo yake uliendeshwa kwa uwazi, haki na uhuru?
“Viongozi wa dini tuliokabidhiwa kondoo wa Bwana kuwachunga na kuwalisha, tukiongozwa na ukweli na kulinda utu wa mwanadamu, katika kikao hiki tupate nafasi ya kutathmini vizuri yaliyopita.
“Waheshimiwa viongozi wa dini na wengine mlioalikwa, kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa TEC, sisi ni walezi wa kiroho na walinzi wa kimaadili. Dhamira ya jamii ni juu yetu kulinda umoja katika taifa letu,” alisema.
Alisisitiza kwamba, wao ni sauti ya kinabii inayotetea haki za kibinadamu pia ni sauti ya wale wasioweza kusema, wanaonyimwa haki zao za misingi kama ile ya kupata viongozi kwa njia ya haki, hivyo aliwataka kutathmini hali ya uchaguzi ulivyokwenda, maandalizi na mipango ya awali yalihusisha kwa kiasi gani wapigakura na vyama husika.
“Maofisa husika walikuwa na maadili kiasi gani katika suala la usimamizi? Uandikishaji wapigakura ulikwendaje? wananchi walikuwa na elimu ya kutosha? Mchakato wa uteuzi wagombea ulikwendaje? Mazingira ya kufanya kampeni yalikuwa sawa kwa wagombea wote na mazingira na vituo vya kupigia kura yalikuwa huru?” alisema.
Pia aliwataka kutathmini kama hatua ya kuhesabu na kutangaza matokeo zilifanyika bila kuleta maswali yoyote.
“Lengo hapa si kutafuta makosa. Sehemu ambayo uchaguzi ulikwenda vizuri tupongeze na tuchukue kama kiwango cha kufanya vizuri zaidi siku zijazo,” alisisitiza.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED