VAR Mobile ndizo zitakuwa mwarobaini wa Ligi Kuu Bara

Nipashe
Published at 01:20 PM Dec 16 2024
VAR Mobile
Picha:Mtandao
VAR Mobile

NI wazi kuwa msimu wa 2024/25 Ligi Kuu Tanzania Bara itamalizika bila kuwa na Teknolojia ya Video ya kumsajili Mwamuzi, VAR.

Hii ni tofauti kabla ya kuanza msimu ambapo viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB), walisema teknolojia hiyo itatumika nchini.

Mtambo wa VAR ukaletwa na kufungwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, tukaambiwa pia kuwa wadhamini wanaoonesha ligi hiyo watanunua mtambo wa VAR ambao unatembea (VAR Mobile), ambao utakuwa unakwenda popote pale nchini ambapo mechi inachezwa.

Bosi mmoja wa TFF alisema watatengeneza kanuni ambayo inafanya mechi mbili za ligi ziwe zinatumia VAR, na hasa zile zenye mvuto wa mashabiki kama za Simba na Yanga.

Alikuwa na maana kama Yanga inacheza Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambako kumefungwa VAR, Simba ikienda kucheza Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza basi ile VAR Mobile inatakiwa iende huko.

Bahati mbaya sana tayari imetangazwa kuwa hakutakuwa na VAR kwa sababu mbalimbali, kwani baadhi ya waamuzi ndiyo kwanza wapo kwenye mafunzo.

Kwa maana hiyo mpaka watakapomaliza kusoma, mzunguko wa pili tayari utakuwa umeshaanza, hivyo hakuna ulazima wala umuhimu wowote wa kutumia teknolojia hiyo, hivyo msimu ujao teknolojia hiyo inaweza kuanza kutumia.

Hata hivyo, nimemsikia Rais wa TFF, Wallace Karia, akisema moja ya changamoto ni kwamba viwanja vingi nchini havina miundombinu ya kufunga na kutumia VAR.

Ni kweli kabisa, kwa maana hiyo kama kweli msimu ujao Tanzania inataka kutumia VAR kwenye mechi zake za ligi kunatakiwa mjadala kwa wadau wa soka na watoke na msimamo wa pamoja.

Kwanza kabisa ieleweke kuwa ili ligi iwe bora na iwe ya haki ni lazima mechi zote zitakazochezwa zinapaswa ziwe na VAR.

Haiwezekani mechi inazocheza Simba, Yanga ziwe na VAR, halafu Pamba Jiji inacheza na KenGold hakuna teknolojia hiyo. Hiyo si haki na haileti ile maana ya mchezo wa soka 'fair play'. Kama nchi inataka kuwa na VAR, viwanja vyote nchini vifungwe teknolojia hiyo, kama haiwezekani basi ligi ichezwe tu bila kuwapo ili mradi tu kila mechi ichezeshwe sawa na nyingine. Ninaamini hakuna mechi bora kuliko nyingine kwenye ligi.

Timu zote zinataka ubingwa na zingine zinataka zibaki Ligi Kuu, na baadhi zinajinasua kushuka daraja, hizo zote zinahitaji maamuzi ya haki na ya uangalifu.

Ndiyo maana narudia kusema mjadala wa wadau wote wa soka nchini unatakiwa, kama kweli wanahitaji ligi yenye matabaka ya maamuzi yenye VAR, au yenye haki sawa kwa wote.

Mimi nadhani kwa hali hii, msimu ujao TFF na wadhamini wajitahidi kupata VAR Mobile nyingi ambazo zinaweza kumaliza tatizo hilo na si za kufunga.

Kama bado viwanja vingi hapa nchini vina mapungufu au miundombinu yake ni hafifu kufunga mitambo hiyo, basi hakuna haja ya kuleta VAR ya kufunga, badala yake zile zinazohamishika ambazo zitakuwa zipo kwenye magari tu kama ile ambayo imeahidiwa na wadhamini.

Nadhani aina hizi za VAR ndizo zitakazoifaa nchi yetu kutokana na aina ya viwanja vyetu mpaka hapo vitakapoboreshwa kuwa vya kisasa zaidi.