Hoja ya kada CCM yazua jambo

By Mussa Mwangoka , Nipashe
Published at 01:45 PM Dec 16 2024
Bendera ya CCM
Picha:Mtandao
Bendera ya CCM

KAULI ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mbunge mstaafu wa Mpanda Mjini, Said Amour Alfi kwamba ni makosa makubwa kushabikia kukandamiza upinzani katika uchaguzi nchini, imezua jambo:

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Katavi, Teonas Kinyoto amedai kauli hiyo haiakisi uhalisia wa siasa zinazofanywa na chama hicho kikongwe nchini na anashangaa kutolewa na mwanasiasa huyo.

"Unajua siasa za CCM ni za kushindana kwa hoja na sera nzuri, ndizo zinazofanya ikubalike na kupata ushindi kwenye uchaguzi mbalimbali inaoshiriki. Shida ni kwamba hivi vyama vya upinzani havijipangi kikamilifu kushindana na CCM ambayo ina sera madhubuti," alidai.

Alitolea mfano Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27 mwaka huu, akieleza kuwa kuna vijiji 40 vyama vya upinzani havikusimamisha wagombea mkoani Katavi. Alitaja hali hiyo ni ishara kwamba "bado wanajitafuta".

Alisema hoja ya baadhi ya watendaji wa serikali waliosimamia uchaguzi kuruhusu kura feki kuingizwa katika masanduku na watu wasio na sifa kupiga kura, si za kweli kwa kuwa vyama vyote vya siasa viliweka mawakala wa kuangalia mchakato wa zoezi la upigaji kura na walitia saini fomu za kukubali matokeo.

Mwenezi huyo alipoulizwa kama kuna hatua zitachukuliwa dhidi ya mwanasiasa huyo kutokana na kauli yake hiyo, alisema chama kina taratibu zake, lakini kwa sasa hawezi kuzungumza lolote.

Wiki iliyopita, katika mazungumzo maalumu na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Mpanda, Alfi ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa na kuhudumu ubunge wa Mpanda kwa zaidi ya miaka 10 kupitia CHADEMA kabla kurejea CCM, alisema:

"Sisi Chama Cha Mapinduzi tutafanya makosa makubwa sana kama tutatumia rasilimali zetu, nguvu zetu na maarifa yetu kuua upinzani! Lazima tuache upinzani ukue, una faida nyingi sana katika ustawi wa taifa hili."

Alitolea mfano kuwa wakati wa utawala wa awamu ya nne, mikoa ya Kanda ya Magharibi kwa maana ya Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma ilikuwa haijafunguka kimiundombinu, hivyo kutofikika kiurahisi. Nguvu ya vyama vya upinzani ilisaidia serikali kuifungua mikoa hiyo kimiundombinu.

Alisisitiza upinzani ni kichocheo cha maendeleo na ni fursa kwa serikali kukosolewa na hivyo kurekebisha upungufu uliopo na hatua stahiki zikachukuliwa.

Kada huyo wa CCM alisema serikali awamu ya tano ilijielekeza "kuumaliza upinzanina ilifaulu kufanya hivyo", hali aliyoitaka imesababisha kutokuwapo watu au wanasiasa wanakosoa, kitu ambacho kwa mtazamo wake ni hatari kwa ustawi wa maendeleo ya taifa.

"Niwaeleze wana CCM wenzangu; tutakuwa tukijidanganya kama tutaamini kwamba tumeua upinzani. Kiuhalisia upinzani hauonekani ila umo katika mioyo ya watu... tusijidanyanye," alitoa tahadhari. 

Aliweka wazi kuwa yeye binafsi hakufurahishwa na mchakato mzima wa uchaguzi huo, ikiwa pamoja na matokeo yake. Alidai watendaji wa serikali walifanya mambo ambayo anaamini hawakuagizwa na CCM bali kwa matakwa yao binafsi tu wakawakandamiza wapinzani.