Simba ni hatari kwa Mkapa mechi CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:14 PM Dec 16 2024
Bao la dakika ya nane ya nyongeza lililofungwa na winga, Denis Kibu.
Picha: Simba
Bao la dakika ya nane ya nyongeza lililofungwa na winga, Denis Kibu.

BAO la dakika ya nane ya nyongeza lililofungwa na winga, Denis Kibu, liliiwezesha Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia kwenye mchezo wa Kundi A raundi ya tatu, Kombe la Shirikisho Afrika, uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana na kuendeleza rekodi yake nzuri inapocheza kwenye dimba hilo mechi za kimataifa.

Wakati mashabiki wote waliokuwa uwanjani hapo  wakidhani mechi hiyo ingemalizika kwa sare ya bao 1-1, pasi ndefu iliyopigwa na Yusuph Kagoma, ikamkuta Kibu ambaye alipiga kichwa cha kiufundi, mpira ukionekana kama unatoka nje, huku kipa Aymen Dahmen akiwa anautazama tu, mpira ukakwama ndani ya wavu na kuibua shangwe na hoi hoi kutoka kwa mashabiki wa Simba.

Kwa hasira, mashabiki wachache wa timu hiyo ya Tunisia walianza kung'oa viti vya uwanjani hapo na kuvitupa chini, huku wachezaji na viongozi wa timu hiyo wakienda kuwavaa waamuzi kwa madai kuwa wamezidisha muda.
Hata hivyo, kwa muda mrefu wachezaji wa CS Sfaxien walionekana kupoteza muda mara kwa mara kitu ambacho kilisababisha mwamuzi kuzifidia.

Katika mchezo huo, mabao yote ya Simba yalifungwa kwa kichwa na Kibu, katika kila kipindi.

Bao la kwanza alilifunga dakika ya saba ya mchezo akiunganisha faulo iliyopigwa kwenye wingi ya kulia na Jean Charles Ahoua iliyomkuta mfungaji na kuruka juu kuukwamisha wavuni bila kukabwa na mchezaji yoyote wa CS Sfaxien, huku mabeki wake macho yao yakiwa kwa Leonel Ateba.

Bao hilo lilikuwa ni la kusawazisha baada ya kushtukizwa kwa bao la dakika ya tatu ya mchezo, likipachikwa na Hazem Haj Nassem kutokana na makosa ya beki Che Fondoh Malone.

Beki huyo akiwa ameumiliki mpira kwenye wingi ya kushoto, alitaka kumrudishia kipa wake Moussa Camara, lakini haukwenda mbali, badala yake straika huyo aliuwahi na kuukwamisha wavuni, licha ya juhudi za kipa kutokea kutaka kuuzuia.
Bao hilo lilionekana kuwashtua si wachezaji tu, bali hata mashabiki waliokuwa uwanjani, kwa bahati nzuri iliwachukua dakika nne tu Simba kusawazisha.

Simba ilionekana kuamka na kucheza kwa kasi dakika tano za mwisho na za nyongeza ambapo ni wao wenyewe tu walikuwa wakikosa mabao.

Kuingia kwa baadhi ya wachezaji kipindi cha pili kulionekana kuiamsha, baada ya kucheza kwa kasi ya chini kipindi cha kwanza.

Wachezaji walioingia kipindi cha pili ni Joshua Mutale aliyechukua nafasi ya Ahoua, Kagoma, akichukua nafasi ya Debora Fernandes Mavambo, Steven Mukwala aliyetwaa nafasi ya Ateba, Chamou Karaboue, akichukua nafasi ya Che Malone, na Valentin Nouma ambaye aliingia nafasi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Baada ya ushindi huo, Simba imepanda hadi nafasi ya pili nyuma na CS Constantine ya Algeria, ikifikisha jumla ya pointi sita sawa na vinara hao ambao jana usiku walitarajia kucheza nchini Angola dhidi ya Bravo do Maquis ambayo ilishuka hadi nafasi ya tatu, huku Watunisia hao wakibaki mkiani wakiwa hawana pointi, wao na Simba wakicheza michezo mitatu.

Katika mchezo wa jana, Simba itabidi ijilaumu yenyewe kwa kushindwa kuwa mbele dakika 45 za mwanzo licha ya kumiliki mpira kutokana na wachezaji wake kutocheza kwa kasi, badala yake walikuwa wakicheza taratibu na pasi fupi fupi zisizokuwa na maana yoyote.

Ateba alipigwa kichwa kilichotoka nje akiunganisha krosi ya Awesu Awesu dakika ya 26, lakini pia akishindwa kukwamisha mpira wavuni dakika ya 33 na 34.

Dakika moja kabla ya mpira kumalizika, golikipa wa Simba, Camara, alifanya kazi ya ziada, alipochupa na kupangua shuti kali la Habessi Achref, ambaye alipigiwa mpira mrefu kutoka nyuma na kufanya shambulizi la kushtukiza.
Kabla ya kuingia kwa bao la ushindi, Simba ilikosa mabao dakika ya 89 kupitia kwa Joshua Mutale, shuti lake likipanguliwa na kipa Aymen, na dakika tatu baadaye Shomari Kapombe nusura afunge bao, lakini kipa huyo alikaa imara na kuokoa.