Rupia yuko tayari kutua Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:25 PM Dec 16 2024
Elvis Rupia.
Picha:Mtandao
Elvis Rupia.

KINARA wa mabao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Elvis Rupia, amesema atakuwa tayari kujiunga na Simba kama kweli wanamhitaji na watapitia kwenye njia sahihi za kuongea na klabu yake ya Singida Black Stars, kwani hakuna mchezaji yeyote nchini ambaye hataki kuichezea timu hiyo.

Rupia, raia wa Kenya, alisema hayo juzi kutokana na tetesi kuwa Klabu ya Simba inataka saini yake kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

"Mpaka sasa binafsi sijapata ofa kutoka klabu yeyote, labda inaweza kuja baadaye, ukweli hakuna mchezaji yeyote nchini ambayo haipendi kucheza Simba au Yanga, ikitokea ofa na nikakubaliana nayo naweza kwenda," alisema mchezaji huyo.

Habari kutoka ndani ya Klabu ya Simba zinasema kuwa inamhitaji mchezaji huyo kwa ajili kuongeza nguvu kwenye kikosi cha timu hiyo nafasi ya ushambuliaji ambayo ina Leonel Ateba, Steven Mukwala na Valentino Mashaka.

Hata hivyo, wakati Simba ikionesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji huyo, habari zinasema kuwa Yanga nayo ina mpango wa kupiga hodi kwenye klabu hiyo kuulizia huduma ya mchezaji huyo ambaye amefikisha jumla ya mabao saba ya kufunga kwenye Ligi Kuu, akimpiku straika wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu, aliyeongoza kwa muda mrefu akisalia na mabao sita.

Akizungumzia siri ya kupachika mabao, Rupia alisema ni kufanya mazoezi kwa bidii na amejiwekea malengo ya kufunga bao moja katika kila mechi, ingawa baadhi ya michezo ameshindwa kufanya hivyo.

"Kulingana na jinsi ninavyofanya mazoezi, nimekuwa nikijiwekea malengo angalau nifunge bao moja kila mchezo, ila kuna wakati haitokei, nashukuru kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji nimefunga mabao yote mawili nikaipa ushindi timu yangu ya mabao 2-1, sikujua kama nitafunga mawili, moja limeongezeka.

"Ni furaha sana kwa sababu kila straika anataka kuwa hapo juu, kila mmoja anapambana anavyoweza aweze kufika hapo.

"Binafsi natarajia kuendelea kufunga mabao mengi, huko mbele ndiyo tutajua ni nani atakuwa mfungaji bora," alisema Rupia.