WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku tatu kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa upanuzi wa barabara ya Ubungo - Kimara, kuongeza idadi ya wataalamu, vibarua na kufunga taa nyakati za usiku, ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Pia amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Aisha Amour kuwasimamia makandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, ili wafanye kazi usiku na mchana kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam alipozuru na kukagua mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hasan kuongoza wizara hiyo.
Akiwa katika ziara hiyo, Ulega aliagiza ujenzi wa miundombinu hiyo uende sambamba na uwekaji taa za barabarani kwa ajili ya ulinzi na usalama na kupendezesha mandhari ya jiji hilo.
Pamoja na mambo mengine, Ulega hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa BRT awamu ya kwanza inayoanzia Ubungo hadi Kimara ambao hadi sasa umefikia asilimia 26.
"Ni ukweli usiopingika kwamba kipande hiki cha kutoka Ubungo - Kimara ni kisumbufu mno, foleni ni kubwa sana, watu wanateseka na kupata adha, hivyo mkandarasi fanya kazi usiku na mchana, umechelewa sana na hatutaki kuona watu wanataabika hapa," aliagiza.
Pia alisisitiza kutowavumilia makandarasi wazembe wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa wakati na kuahidi kuwachukulia hatua za kimkataba na wengine kutopatiwa kazi nyingine za ujenzi nchini.
Vilevile, alisema hajaridhishwa na maendeleo ya ujenzi miundombinu ya BRT awamu ya tatu inayoanzia katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la Mboto unaotelelezwa na mkandarasi Sinohydro kwa Sh. bilioni 231 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Machi mwakani.
Mbunge wa Ukonga na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, akiwa katika ziara hiyo, alisema ujenzi wa mradi wa BRT awamu ya tatu ukikamilika, utaongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi wa Ukonga na kupunguza muda wa usafiri kutoka saa mbili kwa magari ya kawaida hadi dakika 45 na kwa mabasi ya mwendo kasi dakika 30.
Msimamizi wa miradi ya ujenzi wa BRT kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Frank Mbilinyi alisema mradi wa BRT ulibuniwa mwaka 2004 chini ya Halmashauri ya Jiji kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED