Mazembe yampa kiburi Ramovic

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:19 PM Dec 16 2024
 Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.

BAADA ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya TP Mazembe, ikirudisha bao dakika za majeruhi, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema mechi ya juzi ilikuwa ndiyo bora zaidi kucheza kwa kiwango kizuri kwa siku za karibuni, akizionya timu za Ligi Kuu kuwa dawa yao ipo jikoni.

Akizungumza baada ya mechi hiyo ya raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi, uliochezwa Uwanja wa Mazembe uliopo Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasin ya Congo, kocha huyo alisema timu yake ingeweza kushinda hata mabao matatu au manne kutokana na nafasi zilizotengenezwa, lakini walishindwa kuzitumia.

“Tangu nimefika Yanga nadhani huu ndiyo mchezo wetu bora zaidi kuwahi kucheza, tulifanya vitu vingi kwa usahihi na tulimsoma vema mpinzani, nadhani tulipaswa kufunga mabao matatu au manne kwa nafasi tulizotengeneza.

Tulimiliki mchezo, nimefurahi kwa hiki kilichofanyika, wapinzani wetu walituachia nafasi ya kuchukua mpira katikati bila upinzani, lakini pasi za mwisho nyingi hazikuwa sahihi, na chache zilizokuwa sahihi hazikutumika, inabidi kuboreshe hili, nawapongeza wapinzani kwa kutupa mechi nzuri," alisema kocha huyo ambaye ni mchezo wake wa tatu kuiongoza Yanga kwenye michezo ya kimataifa.

Katika mchezo huo, bao la TP Mazembe lilifungwa na Cheick Fofana dakika ya 42, kabla ya Dube kusawazisha dakika za majeruhi wakati mashabiki wa timu mwenyeji wakiwa wanaamini kuwa timu yao ingeibuka na ushindi.

Yanga ilimiliki zaidi mchezo kipindi cha pili hasa baada ya kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji, Dube aliyechukua nafasi ya Kennedy Musonda, Stephane Aziz Ki, aliyeingia badala ya Maxi Nzengeli, Clement Mzize, aliyeingia badala ya Mudathir Yahaya, na Clatous Chama aliyechukua nafasi ya Duke Abuya.

Hata hivyo, pamoja na ushindi huo, bado Yanga inaburuza mkia ikiwa na pointi moja, TP Mazembe ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake mbili.

Timu ya Al Hilal Omdurman inaliongoza Kundi A, ikiwa na pointi tisa, baada ya juzi usiku kupata ushindi wa bao 1-0 ikiwa ugenini, Uwanja wa Julai 5 nchini Algeria, dhidi ya MC Alger, bao lililofungwa na Guessouma Fofana dakika ya 76.
Al Hilal imeshinda michezo yake yote mitatu iliyocheza, huku MC Alger ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne mpaka sasa.

Wakati hayo yakiendelea kocha huyo amesema sasa anarejea kwenye michezo ya Ligi Kuu, akisema anakuja na mfumo tofauti na aliowaelekeza wachezaji wake dhidi ya TP Mazembe.

Alisema anafanya hivyo kwa sababu kwenye Ligi Kuu timu zinacheza tofauti na michezo ya kimataifa inavyochezwa.

"Huku unaweza kupata nafasi ya kumiliki mpira wakati mwingine bila kubugudhiwa, kwenye Ligi Kuu timu nyingi zinakabia chini na hazitoi nafasi, nakwenda kutengeneza mpango mkakati wa kucheza aina hizo za mechi, hatuwezi kucheza kama hivi tulivyocheza na TP Mazembe," alisema kocha huyo.

Yanga inatarajia kurejea kwenye mechi za Ligi Kuu, Alhamisi wiki hii itakapocheza dhidi ya Mashujaa FC, mechi inayotarajiwa kupigwa, Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.