RIPOTI MAALUMU: Makaburi jirani na madarasa yanavyowagharimu wanafunzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:11 PM Dec 16 2024
Sehemu ya eneo la makaburi karibu na madarasa ya Shule ya Msingi Lipumba, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Sehemu ya eneo la makaburi karibu na madarasa ya Shule ya Msingi Lipumba, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma.

MADARASA yako karibu na makaburi. Kwahiyo makaburi yako karibu na madarasa. Inabidi uchukue muda kufanya utafiti: ni makaburi yaliyofuata shule au shule iliyofuata makaburi!

Vyovyote ilivyokuwa na iwavyo sasa, wakati wa maziko masomo shuleni husitishwa na kulazimu walimu kuungana na wanakijiji katika shughuli za maziko.

Hii ni Shule ya Msingi Lipumba, katika kata ya Kihansi Mahuka, wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma. Ni shule inayomilikiwa na serikali. Namba za usajili: EM 5149. Ilianza kutoa huduma mwaka 1975, yaani miaka 49 iliyopita.

Shule hii iko umbali wa Km 18.1 kaskazini mwa mji wa Mbinga. Mtu anapoanza safari kutoka mjini Mbinga kupitia barabara ya lami ya Mtwara – Mbamba Bay, ni mwendo wa dakika 22 kwa basi.

Matatizo mengi yanakabili shule hii: ina uhaba wa miundombinu. Michache iliyopo imechakaa. Madarasa yako jirani na makaburi ya kijiji, umbali wa hatua 15 tu kutoka kwenye madarasa. 

Hii imefanya kila kinachoendelea makaburini kuwa sehemu ya kinachotendeka darasani; na hata kijamii, walimu wanaofundisha shuleni hapo –  mara zote katika ujirani mwema –  wamebaki kuwa washiriki hai wa matukio yote kijijini – yakiwamo maziko.

Ndani ya mazingira hayo, mwanafunzi anashirikishwa mambo ambayo hakupaswa kuhusika nayo kulingana na umri wake, yakigusa pia imani za kidini, hata kijamii.

Mwanakijiji Samuel Samuel (22), aliyehitimu shuleni hapo miaka 10 iliyopita, anaeleza uzoefu wake, kunapokuwa na maziko kwenye makaburi jirani na shule, walimu wachache hubaki shuleni kuwadhibiti wanafunzi wasipige kelele wala kuchungulia na wengine huungana na wanakijiji kwenye maziko. 

Anasimulia katika mazingira hayo ya kudhibitiwa darasani, anakumbuka namna wao walivyokuwa wanapambana na walimu wao kujaribu kuona kinachoendelea makaburini, ukiwa ni mvuto utokanao na utashi wao wa kitoto.

Hatua hiyo ya walimu kwenda makaburini, inatolewa ufafanuzi na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Denis Malekano (54), anayesimulia katika dhana ya ujirani mwema, walimu ni sehemu ya wanakijiji, hivyo huwajibika kushiriki maziko, wakisitisha jukumu lao la msingi la kufundisha wanafunzi. Masomo yanapisha maziko!

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu Malekano, shule hiyo hivi sasa ina wanafunzi 451 (wasichana 229). Walimu wao ni 12 (tisa ni wa kike).

Mwanakijiji Mzee Samuel Nchimbi (61), anayejitambulisha kwa kauli "nina wajukuu 13 wanaosoma katika shule hii (wanane ni wasichana)", anachangia hoja hiyo kwa kutumia uzoefu wake wa muda mrefu, akisema:

"Kuna kipindi kunakuwa na maziko karibu kila wiki. Inakuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kwa sababu wakati wa maziko, vipindi vyote vya masomo vinasitishwa shuleni, walimu wanajumuika nasi hadi tunapokamilisha shughuli hiyo."

Mzee Nchimbi ambaye ni baba wa mhitimu wa shule hiyo, kijana Samuel, anarejea historia tangu zama walizoikaribisha shule hiyo katika kashikashi za msukumo wa Ujamaa Vijijini, akiwa na simulizi:

"Mimi nimezaliwa hapa Lipumba, nimeyakuta makaburi haya. Historia yake ni kwamba, kulikuwa na eneo lenye ukubwa wa ekari 60. Lilikuwa chini ya wamisionari. Mwaka 1975, likagawanywa -- ekari 42 zikatengwa kuwa eneo la shule ya msingi na ekari 18 zikatengwa kwa ajili ya kanisa la RC (Roman Catholic) na makaburi."

Hata hivyo, Mzee Nchimbi anabainisha kuwa mwili wa kwanza kuzikwa katika eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya makaburi ya kijiji, ulizikwa mwaka 1932, kipindi hicho eneo likiwa chini ya wamisionari. Makaburi yalitangulia shule!

"Uzikaji ulikuwapo hata kabla ya kugawa eneo hili. Mtu wa kwanza kuzikwa katika makaburi haya ni Yombayomba Mpiti ambaye ni babu wa babu yangu. Huku kwa lugha yetu tunamwita "mtete".

"Eneo hili la makaburi linatumika kusitiri miili ya watu wa hapa kijijini Lipumba. Na hakuna ubaguzi; wakristo, waislamu, wote wanazikwa hapa. Mimi mwenyewe ni Mashahidi wa Yehova, lakini nikifa nitazikwa hapa."

Mwenyekiti wa Kanisa Katholiki Lipumba, Parokia ya Kigonsera, Jimbo la Ruvuma, Augustino Msuha, anaungana na mwanakijiji mwenzake, Mzee Nchimbi kwamba madarasa ya Shule ya Msingi Lipumba kuwa karibu na makaburi hayo kuna madhara kwa wanafunzi.

"Walimu wanapositisha vipindi na kuja huku makaburini kuzika ni usumbufu kwa watoto na hali hii ina madhara kitaaluma na kisaikolojia kwa wanafunzi. Msiba unamwumiza hata mtu mzima, wale watoto (wanafunzi) wanakuwa katika hali mbaya zaidi.

"Sisi (kanisa) hivi sasa hatuna uwezo wa kujenga ukuta kutenganisha makaburi na madarasa, lakini tumeamua kupanda miti mpakani mwa shule na eneo la makaburi. Miti hii ikishakua itawazuia wanafunzi kuona kinachoendelea makaburini. Watasikia nyimbo na sala za mazishi, lakini hawataona kinachojiri," anasema Mwenyekiti Msuha.
 
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hii kuhusu idadi ya waliozikwa katika makaburi hayo, Msuha (61) alitoa maelezo yafuatayo:

"Makaburi haya ni ya kijiji, lakini yako chini ya kanisa tangu miaka ya 1930. Jamii yote ya Lipumba inazikwa hapa. Ni vigumu kujua idadi ya waliozikwa hapa mpaka sasa kwa sababu uzikaji ulianza zamani mno.

"Kuna kipindi tunapochimba, tunakutana na mafuvu, maana yake ni kwamba eneo hilo ulizikwa mwili wa binadamu zamani sana. Baadhi ya makaburi yameshafutika, yanayoonekana kwa urahisi ni haya yaliyojengewa. Ni maelfu ya watu wamezikwa hapa, eneo hili la makaburi ni kubwa, ekari 18."  

Wakati kukishuhudiwa hali hiyo shuleni Lipumba, Mwongozo wa Uthibiti wa Ubora wa Shule uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Juni mwaka huu, unaelekeza shuleni kufanyike tathmini yakinifu ya kimazingira, kijamii na kihisia katika muktadha wa elimu.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, uhakiki huo unapaswa kujumuisha muundo wa miundombinu na hali ya jumla ya shule. Lengo ni kuhakikisha mazingira ya shule yanakuza hali chanya, jumuishi na salama kwa ufundishaji na ujifunzaji wenye ufanisi.

Aya ya 4:11 ya mwongozo huo inaelekeza shule na walimu kujenga mazingira rafiki kwa watoto kujifunza na kucheza kwa usalama.

Vilevile, Aya ya 38 ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 (marejeo ya mwaka 2023), inaelekeza serikali ihakikishe inatengeneza mazingira salama na rafiki katika taasisi za elimu na mafunzo nchini.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lipumba, Mathias Mpangala anakiri mazingira ya sasa shuleni Lipumba, hasa katika eneo hili la makaburi kuwa jirani na madarasa, yanakinzana na sera na miongozo ya utoaji elimu nchini.

"Shule hii ni kongwe. Madarasa yake yamechakaa kiasi kwamba hayahitaji kukarabatiwa, bali kubomolewa na kujengwa upya. Kwa kutambua kwamba yalijengwa karibu na makaburi, hivi sasa madarasa mapya tunayojenga tunahakikisha yanakuwa mbali na makaburi.

"Tumekubaliana na wanakijiji kila mwaka walau tujenge darasa moja lenye vyumba viwili na ofisi ya walimu. Tayari wanakijiji wamechangia ujenzi wa darasa moja, ujenzi wake umefikia hatua nzuri, kilichobaki ni kumalizia sakafu na lipu.

"Lengo letu ifikapo mwaka 2026, tuwe na madarasa mapya manne katika shule yetu yenye vyumba viwili na ofisi moja ya walimu kwa kila darasa.

"Halmashauri nayo mwaka jana ilitupatia fedha za kujenga darasa moja, Sh. milioni 40. Ujenzi wake umefikia hatua ya kuezeka. Madarasa haya mapya yanajengwa umbali wa mita 200 kutoka mpaka wa shule na eneo la makaburi. Lengo letu madarasa yatoke kule karibu na makaburi," anasema Mpangala.

Ibara ya 8(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inaelekeza "wananchi watashiriki shughuli za serikali yao kwa mujibu wa Katiba hii". Je, wakazi wa kijiji cha Lipumba wanashiriki vipi kunusuru shule yao?

Mwanakijiji Remista Ndunguru (46) anasema kuwa mwaka 2022 walikubaliana katika kikao cha kijiji wachangie Sh. 20,000 kwa kila kaya yenye mke na mume au Sh. 10,000 kwa kaya yenye mzazi mmoja.

Ndilo fungu ambalo Ofisa Mtendaji Mpangala anajivunia linatumika katika ujenzi unaoendelea wa darasa lenye vyumba viwili na ofisi ya walimu.

Remista anayejitambulisha ni mama wa watoto watatu wanaosoma shuleni Lipumba (mmoja wa kike yuko darasa la sita na wawili wa kiume wanaosoma darasa la nne na la awali), anasema:

"Kama mzazi nina uchungu na ile hali iliyoko shuleni kwa wanangu. Muda wa kuzika, walimu wachache wanaobaki shuleni, hupita kila darasa kutoa tahadhari watoto (wanafunzi) wasipige kelele. Kunakuwa na ukimya shuleni mpaka pale maziko yanapokamilika.

"Ni hali inayowajengea woga wanafunzi. Yaani mtoto yuko darasani lakini anaogopa kinachoendelea makaburini. Hali hii inawaletee shida wanafunzi kifikra. Siku ya maziko wanafunzi ni kama hawasomi kabisa, maana kunakuwa na pitapita ya watu shuleni wanapokwenda makaburini, pia wakati wa kutoka makaburini."

Ofisa Elimu Msingi Halmashuri ya Wilaya ya Mbinga, Veronica Justine, alipotafutwa na mwandishi wa habari hii Novemba 24 mwaka huu kuzungumzia kinachojiri katika shule hiyo, alisema:

"Ninatambua changamoto zinazoikabili Shule ya Msingi Lipumba, lakini msemaji wa halmashauri ni mkurugenzi. Nikizungumzia suala hili, nitakuwa ninakiuka taratibu."

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, alipotafutwa na mwandishi wa habari hii kuzungumzia suala hilo, alitoa ufafanuzi ufuatao:

"Nina taarifa kuhusu changamoto ya miundombinu katika shule hiyo. Nina shule za msingi 168, nyingi zilijengwa zamani, majengo yake yamechakaa kama hiyo ya Lipumba.

"Kuhusu maziko kuingilia ratiba ya masomo shuleni, nitawasiliana na Ofisa Elimu Msingi (Veronica) ili kupata taarifa kamili ya suala hilo kabla ya kulizungumzia kwa undani."


*ITAENDELEA KESHO