MAMLAKA ya Mapato Tanzania ( TRA)mkoa wa kikodi Tegeta imesema itaendelea kutoa elimu kwa walipa kodi na wafanyabiashara ili waone umuhimu wa kulipa kodi hiyo kwa hiari kukuza pato la nchi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Msaidizi wa Ukaguzi na Uhiari wa Ulipaji Kodi, Maigloria Saria, baada kuwatembelea walipakodi eneo la Goba wilaya ya Kinondoni.
Alisema Mamlaka hiyo inaendelea kusogeza huduma hizo kwa Wafanyabiashara wa mkoa huo ili kuwarahisishia na kuepuka kupoteza muda mwingi kusafiri hadi Makao Makuu
"TRA katika kampeni yake ya mwezi huu wa Desemba tumelenga kuendelea kutoa elimu na kurudisha asante kwa walipa kodi wetu, kuwasikiliza na kuchukua maoni yao katika kuelekea mwaka mwingine hasa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ili kulipa Kodi bila usumbufu,"alisema Maigloria.
Mkurugenzi wa Kampuni ya GAF International Group Limited, Flora Erasto aliipongeza serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara na kuishukuru TRA kwa kutambua kampuni yao kama walipakodi waaminifu na kuahidi kuendelea kufanya vizuri katika eneo hilo la kulipa kodi kwa serikali.
Flora alisema wataendelea kuwa waaminifu katika kutekeleza yale yote ambayo wanatakiwa kufanya katika biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Mafanyakazi wa kampuni ya B&B Specialized Polyclinic, Dk. Bhavin Jani alisema wako tayari kuendelea kuinga mkono serikali kwa kulipa kodi kwa uaminifu na kwa kufuata taratibu na sheria zinazosimamia shughuli za biashara."Tunashukuru sana kwa kuthaminiwa na mamlaka zinazosimamia biashara kwenye nchi yetu, tunahaidi tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili nchi yetu inasonge mbele na maendeleo yapatikane." alisema Dk.Jani
Dk. Jani alikipongeza kitengo cha huduma kwa wateja cha TRA kwa kuongeza ufanisi katika utatuzi wa changamoto za wateja hasa katika kipindi hiki cha mabadaliko ya teknolojia."Naendelea kupongeza TRA kwa kuendelea kuboresha mifumo mbalimbali ya kodi licha ya kuwa hazijaisha zote, mfano ukilipa kodi mfumo unaweza usikutambue kama umelipa kodi lakini hiyo haikufanyi ukashindwa kulipa na unapotoa taarifa kuhusu hilo watu wa huduma kwa wateja wanatatua kwa wakati,"alisema Dk.Jani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED