UWEKEZAJI uliofanywa na Mamlaka ya Bandari (TPA) katika Bandari ya Mtwara umevutia meli nyingi za kigeni katika usafirishaji wa korosho kwenda katika masoko ya kimataifa na kuufanya msimu wa 2024/2025 wa zao hilo la biashara kuwa wa mafanikio.
Mafanikio hayo yanatokana na maboresho ya bandari hiyo yanayofanywa na Serikali katika kusaidia ukuaji wa biashara ya korosho zinazozalishwa katika mikoa ya Kusini kwenye masoko ya kimataifa.
Mmoja wa wafanyabishara wa Korosho mkoani Mtwara, Omega Makanjiro alisema jana kuwa uwekezaji huu umewezesha meli tatu kuhudumiwa kwa wakati mmoja katika gati mpya na ya zamani, jambo lililochangia na kampuni nyingi za meli kupeleka meli zao katika Bandari ya Mtwara na wafanyabishara kusafirisha biashara zao kwa urahisi.
Aliipongeza TPA kwa juhudi za kuboresha huduma katika bandari hiyo na kuishauri iendelee kuitangaza kutokana na huduma zake zilizoboreshwa, ili kuvutia kampuni nyingine za meli zaidi.
Naye, Herman Colman kutoka kampuni ya ETG, alisema msimu huo umekuwa mzuri zaidi kwao, kwani tangu kuanza kwa msimu huu wameshasafirisha tani 40,000, ikilinganishwa na tani 26,000 walizosafirisha katika msimu uliopita.
“Hii inatokana na uboreshaji wa huduma na uwepo wa meli za kutosha katika kutoa huduma tunachukua na kusafirisha mizigo yetu kwa wakati na hii inapunguza gharama kwa mteja, ambaye ndiye mtumiaji wa mwisho,” alisema.
Aliipongeza TPA kwa kuongeza mitambo na mashine za kisasa, jambo lililoongeza ufanisi na uwezo wa kuhudumia shehena nyingi kwa wakati.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, alithibitisha kuwa uzalishaji wa korosho umeongezeka mwaka huu na hadi sasa, wameuza tani 238,000.
Aliongeza kuwa hakuna changamoto yoyote ya meli au makasha ya kubeba korosho kwa msimu huu, tofauti na misimu ya nyuma.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wanunuzi na wasafirishaji ni muhimu ili kuhakikisha msimu huu unakuwa endelevu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuinua hali za wakulima.
Taarifa ya TPA ilisema kuwa hadi mwishoni mwa mwezi Novemba 2024, TPA kupitia Bandari ya Mtwara imeshahudumia shehena ya korosho ghafi tani 133,000 kwa ajili ya masoko ya kimataifa, ongezeko kubwa la tani 72,921, ikilinganishwa na tani 60,079 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023 na kwa mujibu wa TPA, hili ni ongezeko la asilimia 121.
Taarifa ya TPA imeongeza kuwa meli 17 tayari zimefika na kuhudumiwa katika Bandari hiyo na kati ya hizo, 14 zimepakia shehena ya makasha (Container Vessels), huku tatu zikibeba korosho zilizopakiliwa kwa magunia.
Taarifa hiyo ilisema kuwa jumla ya makasha 3,366 tayari yamepakiliwa na kuondoka kutoka Bandari ya Mtwara, kati ya makasha 7,621 yaliyopo katika bandari hiyo kwa ajili ya kubeba zao hilo la biashara.
Ilisema serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 157.8 kuboresho Bandari ya Mtwara na mafanikio haya ni sehemu ya matokeo ya uwekezaji huo.
Ilisema kabla ya uwekezaji huo, korosho zote kutoka Mikoa ya Kusini zililazimika kusafirishwa kwa malori hadi Dar es Salaam ili zisiweze kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED