Dk. Semesi atoa wito wa ushirikiano NEMC

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:40 PM Dec 16 2024
MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Sware Semesi.
Picha:Mpigapicha Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Sware Semesi.

MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Sware Semesi, amewahimiza watumishi wa taasisi hiyo kuimarisha ushirikiano ili kuboresha utendajikazi na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Akizungumza jana katika hafla ya pamoja na watumishi wa NEMC iliyofanyika Bagamoyo, Dk. Semesi aliwataka wafanyakazi kujitoa kwa dhati, kupendana, kuheshimiana, na kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kimazingira ili kufikia malengo ya taasisi. 

Hafla hiyo pia ilijumuisha burudani na michezo mbalimbali iliyolenga kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kikazi.

"2024 ni mwaka wa NEMC kujitafuta na kujitathmini, ulikuwa mwaka wa kutengeneza njia ya kufikia malengo. Ndio maana nilisisitiza umuhimu wa kujuana, kujengana, na kuweka malengo. Mwaka 2025 ni mwaka wa kuchukua hatua na kuyatimiza," alisema Dk. Semesi.

Aidha, alisisitiza kwamba NEMC inapaswa kusimamia dhana ya ushirikishwaji kwa weledi ili kufanikisha malengo makubwa ya kimazingira, kwa kuwa mazingira ni sehemu muhimu ya maisha ya watu.