Msalaba Mwekundu yakamilisha ujenzi wa nyumba 35 za waathirika wa mafuriko Hanang

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:01 PM Dec 16 2024
Katibu Mkuu wa chama hicho, Lucia Pande.
Picha: Sabato Kasika
Katibu Mkuu wa chama hicho, Lucia Pande.

Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kimekamilisha ujenzi wa nyumba 35 zenye thamani ya Shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani Hanang, mkoani Manyara. Mafuriko hayo, yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana, yalisababisha vifo na kuathiri makazi ya watu wengi.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Lucia Pande, alitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari. Lucia alisema kuwa nyumba hizo ni sehemu ya ahadi ya serikali ya kujenga jumla ya nyumba 101 kwa waathirika wa mafuriko hayo.

“Tumeweza kukamilisha ujenzi wa nyumba 35 kati ya zile 101 zilizoahidiwa na serikali. Sisi kama wadau wa serikali tumejitahidi kufanya sehemu yetu kwa kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu haya ya kibinadamu,” amesema Lucia.

Ameeleza kuwa hatua inayofuata ni kukabidhi nyumba hizo kwa walengwa kwa mujibu wa mpango uliopangwa na serikali.

Lucia amebainisha kuwa mwaka huu chama hicho kimetoa huduma za kibinadamu katika maeneo mengi, yakiwemo mafuriko ya Rufiji mkoani Pwani, pamoja na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, Marburg, na Mpox.

“Majanga mengi mwaka huu yamekuwa ya mafuriko, lakini pia tumeendelea kushughulikia magonjwa ya mlipuko. Katika maeneo kama Simiyu na Shinyanga, tumeshirikiana na serikali kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa na kusaidia kupunguza athari za magonjwa hayo,” amesema Lucia.

Ameongeza kuwa chama hicho kimepeleka wafanyakazi wa kujitolea kutoa elimu katika mikoa ya mpakani baada ya kugundulika kwa magonjwa ya mlipuko kama Marburg na Mpox, kwa kushirikiana na wataalamu wa serikali.

Lucia ameeleza kuwa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kimekuwa kikishirikiana na vyama vya Msalaba Mwekundu kutoka nchi mbalimbali, kama Ufaransa na Kenya, ambavyo vimechangia rasilimali fedha na msaada wa kitaalamu kwa ajili ya kuendesha huduma za kibinadamu wakati wa majanga.

“Tunaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha tunatoa huduma bora zaidi kwa Watanzania wote wanaoathiriwa na majanga ya asili na yale ya kibinadamu,” alisema.

Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kimejikita katika kusaidia jamii kwa kutoa misaada wakati wa majanga na kushirikiana na serikali katika mipango ya maendeleo endelevu ya kibinadamu.